UANDISHI WA BARUA-1

Amani Njoka, Swahili hub

Barua ni karatasi iliyoandikwa ujumbe kwenda kwa mtu mwingine ilia pate taarifa fulani mahsusi. Hii ni njia ya mawasiliano inayotumiwa tangu kale ambako wengi waliwasilisha taarifa mbalimbali kwa watu walio mbali. Baada ya barua kuandikwa, ili tumiwa kwa namna yoyote kati ya posta au mtu kuipeleka mkononi na ujumbe kumfikia mhusika.

Hii ndiyo mbinu ya kale zaidi ambako jamii mbalimbali duniani ziliitumia kuwasiliana tangu kugunduliwa kwa maandishi kuanzi Ugiriki ya kale, Asia, Misri na Mashariki ya kati. Ni mchakato ambao ulihusisha barua lakini barua iliandikwa kwa madhumuni tofautitofauti. Miongoni mwa barua hizo ni kama vile:

Barua za Kirafiki, ni barua zinazoandikwa na watu au mtu mwenye uhusino fulani wa karibu au kiirafiki. Barua hizi huandikwa hizi kwa lengo la kupasha, kujuliana hali, kuomba, kushukuru na taarifa nyingine muhimu kwa mtu huyo kuzifahamu. Kulingana na hadhi ya barua hii, inaweza kuandikwa kwa ndugu, rafiki au watu wenye mahusiano mbalimbali katika jamii husika.

Kama zilivyo barua nyinginezo, barua ya kirafiki ina taratibu zilizokitwa katika muundo. Maana yake isipofuata muundo huo haiwezi kukidhi vigezo vya kuwa barua ya kirafiki au barua kwa ujumla. Barua ya kirafiki huwa na muundo ufuatao:

Anwani ya mwandishi, ambayo huandikwa upande wa juu kulia mwa karatasi katika umbo la mshazari. Anwani hii ni mahsusi kwa ajilia ya kumtambulisha mwandishi na kumsaidia mpokeaji kufahamu ilipotoka barua hiyo.

Pia itamsaidia kurudisha majibu kupitia anuani hiyohiyo. Anuani hujumuisha mahali, sanduku la posta na tarehe iliyoandikwa. Mfano, mwandishi anaweza kutaja shule, ofisi, mkoa au mahali pengine na sanduku posta kabla ya kumalizia kwa tarehe.

Mwanzo wa barua, huwa na mianzo maalumu maalumu inayotambulisha wazi kuwa mwandikiwa ni nani kwa mwandishi. Mfano, mpendwa baba, mpendwa mama, mpendwa rafiki au kutaja jina la mhusika. Mwanzo wa barua huandikwa kushoto mwa karatasi chini kidogo baada ya tarehe au anuani.

Kiini cha barua, hiki ni kipengele ambacho mwandishi anatarajiwa kuandika dhumuni la barua huku akitanguliza salamu kwa mwandikiwa. Mfano, mwandishi anaweza kuanza, salamu dada, natumaini u bukheri wa afya, mimi pia sijambo. Pia anaweza kueleza hali yake kwa undani ikiwa anumwa, maendeleo yake ya kazi, shule ikiwa kutakuwa na uhumuhimu wa kufanya hivyo.

Baada ya hapo mwandishi ataeleza sababu ya barua. Hapo atasema, ‘dhumuni la barua hii ni kukujulisha kuwa fedha ya ziada uliyonipa wakati ule imekwisha hivyo naomba unitumie nyingine’ na mambo mengine yanayofanana na hayo kutegemea na mwandishi. Hapo mwandishi atapaswa kueleza mambo yote mpaka ya ziada ambayo pengine hayana kipaumbele kuliko dhumuni kuu. Mwisho wa barua, hii ni sehemu ya mwandishi kumuaga msomaji au mwandikiwa.

Mara nyingi huhitimisha kwa kutuma salamu kwa watu wengine walio upande wa kule barua iendako. Mfano, mwandishi anaweza kuaga kwa kusema ‘wasalimu dada na kaka’ au maneno mengine ambayo yanaonesha kuwa mwandishi sasa anamaliza kuandika barua yake.

Author: Gadi Solomon