Ubalozi wa Tanzania watangaza kufundisha Kiswahili bure

Na Loveness John

Ubalozi wa Tanzania nchini Italia umefungua darasa la Kiswahili katika ofisi zake ikiwa ni utekelezaji wa maazimio saba yaliyotolewa na Makamu wa Rais wakati wa madhimisho ya Kiswahili mwaka huu.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango alitoa maagizo hayo siku ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, huku  akizitaka ofisi zote za ubalozi kufungua madarasa ya kufundisha Kiswahili huku, ubalozi huo wa Italia ukianza mara moja utekelezaji.

Akizungumza kupitia Wabongo Ughaibuni Media, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo amesema lengo la uzinduzi wa darasa la  Kiswahili ndani ya Ubalozi wa Tanzania ni kuwaunganisha watu wanaopenda kujifunza lugha ya Kiswahili na familia ya watu zaidi ya milioni 200 wanaozungumza Kiswahili.

 Amesema kutakuwa na darasa ambalo limezinduliwa ubalozini na kozi zitatolewa bure kwa wanafunzi wanaohitaji kujifunza Kiswahili.

Balozi Kombo amesema 23 Septemba, 2021 kupitia kifungu namba 61 cha mkutano mkuu wa Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni (Unesco) wa 61, Kiswahili kilitambulika kuwa lugha ya kimataifa ulimwenguni.

“Lugha haiwezi kufikia orodha ya kimataifa kama haijakidhi masharti Fulani. Kiswahili kilitimiza masharti hayo yote, sasa inakuwa lugha ya 10 kuzungumzwa katika lugha za kimataifa na kutambulika duniani,” amesema.

Balozi Kombo amesema watu wanaozungumza Kiswahili ni zaidi ya watu milioni 200, hivyo idadi hii inashinda baadhi ya lugha nyingine duniani.

Chuo Kikuu cha Turin ambacho anafundisha Profesa Graziella Acquaviva, ni moja ya vyuo ambavyo vilialikwa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, baada ya kupendezwa na sherehe hiyo wameomba kwa mwaka ujao Siku ya Kiswahili Duniani ifanyike katika Chuo Kikuu cha Turin mjini, Turin ambacho ni chuo kikuu moja wapo kikubwa na cha miaka mingi nchini Italia.

Author: Gadi Solomon