Wabunge kuvaa viatu vya wahusika wakati wa mijadala ya Bajeti

Julius Mnganga, Mwananchi

Juzi, Serikali iliwasilisha bungeni bajeti yake ya Sh33.11 trilioni kwa ajili ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwasilisha bajeti hiyo akisema inakwenda kukidhi mipango ya Serikali, mpira sasa umerushwa mikononi mwa wabunge.

Wabunge wakiwa ndio wawakilishi wa wananchi, wanatakiwa kuvaa uhusika na viatu vya wapigakura waliowatuma kuijadili bajeti hiyo kwa lengo la kuiboresha na kuifanya iwe na maana kwa kila mwananchi.

Ukiacha hotuba ambayo pengine kila mtu ameisoma au kuisikia, wabunge wana fursa ya kuangalia kila senti iliyotengwa kwa kila eneo, kuichambua na kuona kama inastahili, inapungua ni zaidi ya kinachohitajika na kuishauri Serikali.

Watambue kuwa wao ndio jicho la wananchi la kuichungulia bajeti na kuona kama ina manufaa kwao.

Hivyo, waweke pembeni ushabiki na ushindani wa kisiasa, watangulize mbele masilahi mapana ya wananchi na Taifa ili kuhakikisha Bajeti inapitishwa ambayo ina manufaa kwa wote.

Hatutarajii kuona au kusikia, kama ambavyo imewahi kutokea, baadhi ya wabunge wakichangia kwa kuangalia masilahi binafsi au kutoa michango ambayo haiendani na suala zima la bajeti, badala yake tunatarajia kuona mawazo na akili zao zote zikielekezwa katika kuboresha bajeti hiyo. Vilevile, haitakuwa matarajio yetu kuona wabunge wanakwepa wajibu wa kuwatetea waliowatuma na kuisemea Serikali wanayotakiwa kuisimamia kuhakikisha bajeti ni bora na inatekelezwa kama ilivyopitishwa.

Tunaamini kila mbunge anatambua kuwa msingi wa bajeti ni upatikanaji wa fedha, hivyo atumie mwanya huo kuibua vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitaisaidia kupata fedha za utekelezaji wa Bajeti hiyo kama ilivyopangwa.

Serikali nayo kwa upande wake, iwe tayari kupokea mapendekezo ya wabunge na wadau wengine na kuyafanyia kazi badala ya kubaki na mpango wake, ikumbuke kwamba wabunge wanafanya hivyo kwa niaba ya wananchi.

Ikiwa hayo yatafanyika, ni wazi kuwa bajeti itakayopitishwa itakuwa nzuri na inayotekelezeka, badala ya kuwa tu na namba ambazo mwisho wa siku fedha hazipo na mipango inasalia kwenye makaratasi.

Tunasema hivyo tukitambua kuwa miaka mingine bajeti imekuwa ikipitishwa lakini ikifika mwisho wa mwaka husika, inabainika kuwa fedha zilizopelekwa kwenye maeneo yaliyopangwa ni kidogo.

Ndiyo maana tunashauri wabunge watumie vizuri fursa waliyonayo kushauri namna bora ya upatikanaji wa fedha zilizopangwa ili bajeti hiyo itekelezeke.

Katika michango yao, wabunge waangalie namna ya kuishauri Serikali kuishirikisha sekta binafsi katika kukuza uchumi badala ya kuendelea kudhani kwamba Serikali inaweza kufanya kila kitu peke yake.

Ushauri wa namna hiyo unaweza kutuondoa katika dhana kwamba Serikali inapendelea kufanya kazi na taasisi zake pekee, badala yake wahakikishe kila sekta inashiriki kusisimua uchumi wa nchi.

Ili hayo yote yaweze kufanyika kwa ufasaha, inabidi mjadala uwe wa kina na wasimamizi wa mjadala huo wajitahidi kuwa katikati ili mawazo ya kila mmoja na pande zote yaweze kuchukuliwa kwa njia zilizo sawa.

Cha msingi ni wabunge kujiepusha na kauli zinazoonekana wazi zina lengo la kuwagawa kiitikadi wakati bajeti inayoandaliwa ni ya wote na italinufaisha Taifa zima.

Author: Gadi Solomon