Uke wenza

Uke wenza

Litege lako sikio, nipate kusimulia,

Yalonisibu mwenzio, katika hii dunia,

Moyo wanienda mbio, sijui pa kuanzia,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Hadithi yangu ya kweli, leo nakuhadithia,

Yanichanganya akili, kila nikifikiria,

Lengo kukwambia hili, uweze nisaidia,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Kuna bwana mvulana, jina nitakutajia,

Siku aliponiona, moyoni akaingia,

Akaniambia bayana, moyo umekuridhia,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Siku zikazidi kwenda, nikaja mtamkia’

Kwamba nami nakupenda, jibu ninakupatia,

Uendako nitakwenda, wala sitakuachia,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Hapo hakuficha kitu, wazi akaniambia,

Mimi ni mume wa mtu, hivyo nina familia,

Nina watoto watatu, mke amenizalia,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Kubwa aloniahidi, heshima kunilindia,

Hadi ndoa ikibidi, kwa Mola nishuhudia,

Hataki ufisadi, na bughuza za dunia,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Jambo alilonishtua, ni kuhusu yangu dini,

Ka kweli nampenda, kubadili yangu dini,

Bila woga nitamkia, ya haki ndo yangu dini,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Nikaiomba nafasi, wazazi kuwaambia,

Machungu katika nafsi, wazazi walinambia,

Angeoa dini pasi, uke wenza hutowezea,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Sana alinibembeleza, ila nikamkatalia,

Uke wenza sitaweza, nakataa mara mia,

Pia nikamkataza, mkewe kumuachia,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Nimebaki njia panda, mawazo najiwazia,

Sijui wapi pa kwenda, kushoto au kulia,

Anipenda nampenda, nanzaje kumkimbia?

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Kisa ninakikatisha, nashindwa kumalizia,

Mana anihuzunisha, huyu wangu my dia,

Usaliti nihusisha, sishiriki yake dhambi,

Kumpenda nampenda, uke wenza sitaweza.

Shairi hili limeandaliwa na Mtunzi Pelagia Daniel

Kama unashairi unaweza kutuma kwa baruapepe ss.gadner@gmail.com au wasiliana nasi kwa namba 07121127912

Author: Gadi Solomon