Usanifishaji wa Istilahi

Na Nabil Mahamudu


Istilahi ni neno au maneno (msamiati) yanayotumika katika uga fulani maalumu, unaweza ukawa uga wa kimichezo, kitabibu, kisanaa na kiutawala. Idara ya Istilahi na Kamusi katika Baraza la Kiswahili la Taifa ndio yenye kazi ya kukusanya maneno kutoka nyanja mbalimbali ambayo yana uhitaji katika jamii kimatumizi kwa mujibu wa Wema. Msigwa (Mchunguzi wa lugha, Bakita) anabaisha kwamba “kinachofanyika tunakusanya istilahi kutoka lugha mbalimbali huwa mara nyingi tunakusanya istilahi kutoka lugha ya Kiingereza na kuzitafutia visawe, visawe ni yale maneno yanakuwa na maana sawa na msamiati wa lugha ya kiingereza.” alisema Msigwa ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Istilahi na Kamusi, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).
Inapotokea katika jamii msamiati fulani unahitajika labda kuna maneno yamekosekana kwenye jamii na yanatakiwa kuingizwa ili yatumike, Idara ya Istilahi na Kamusi ndio inayohusika kukusanya na kutafuta visawe katika Kiswahili kama vipo, na kama havipo pia inatafuta katika jamii kupitia lugha za kijamii. Baada ya hapo msamiati huo ukishakusanywa hatua inayofuata ni usanifishaji ukisikia usanifishaji unafanyika Bakita kimsingi ni idara hii, kwahiyo ukusanyaji wa istilahi ukimalizika na kuwekewa visawe, hatua inayofuata ni uwasilishaji wa mapendekezo kwenye Kamati ya Kusanifu lugha, kamati hii inajumuisha watu kutoka sehemu tofautitofauti: Tanzania Bara na Visiwani ambapo maranyingi wanakuwa ni Magwiji wa lugha pia kamati hii inahusisha Magwiji wa uga ambao usanifishaji wa istilahi zake unafanyika– Wao wakija kazi inayofanyika ni kujadili msamiati ule, makubaliano yakishafanyika kwamba msamiati unaopendekezwa unaweza kutumika hivyo, kazi wanayoifanya Bakita ni kuunadi msamiati huo ili uweze kupewa kipaumbele katika matumizi ya jamii, Bakita wanaunadi msamiati huo kupitia vyombo vya habari mathalani redio na televisheni kutokana na nguvu ya ushawishi na kuaminika katika vyombo vya habari ndani ya jamii. Kwaujumla huo ni mlolongo wa usanifishaji wa istilahi kutoka nyanja mbalimbali ambao unafanyika chini ya Idara Istilahi na Kamusi ambapo Idara hii ndio ina dhamana ya kazi hiyo kadhalika inahusika na maandalizi ya Kamusi:Kwa mujibu wa kigezo cha idadi ya lugha katika uanishaji wa Kamusi, Kamusi za lugha moja (Kamusi Wahidiya), Kamusi za lugha mbili tofauti inaweza kuwa Kiingereza-Kiswahili au Kiswahili-Kiingereza(Kamusi Thaniya) kadhalika Kamusi ndogo ambazo hizi ni Kamusi maalumu za nyanja mbalimbali:Sheria, Utabibu, Siasa, na Sanaa.
Kwaufupi: Mchakato wa usanifishaji wa istilahi unaofanyika Bakita.
1.Ukusanyaji wa neno au maneno (istilahi) kutoka lugha mbalimbali mara nyingi lugha ya Kiingereza, ambazo zina uhitaji wa matumizi katika jamii.
2.Utafutaji wa Visawe
3.Uswasilishaji wa mapendekezo kwenye kamati ya kusanifu lugha.
4.Bakita kuunadi msamiati kupitia vyombo vya habari ili uweze kutumika katika jamii

Author: Gadi Solomon