Usasa usasambu

Suala la utandawazi limekuwa ni jambo ambalo hatuwezi kuliepuka katika maisha yetu ya kila siku. Lakini suala hili limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kupelekea kuwaathiri kimwili na kiakili. Kuingia kwa utandawazi kumewafanya vijana watumie muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii na intaneti ambako wanajifunza mambo mengi ya hovyo. Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na hata kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto kwani kila anayejaribu kulishika lazima limuunguze. Kwa kuona hayo yote mwandishi wa tamthiliya hii ameamua kuifungua macho jamii ili iweze kuchukua hatamu kuwanusuru watoto hasa wa kike.

Mwandishi William Himu amezaliwa na kukulia mtaa wa Ngarenaro wiliyani Babati mkoa wa Manyara. Alianza kupata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi ya Lang’ata Bora iliyopo wilaya ya  Mwanga mkoa wa Kilimanjaro na kuendelea na  elimu ya Sekondari katika shule ya Lang’ata Bora iliyoko huko huko Mwanga Kilimanjaro kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Air wing iliyopo Ukonga Banana Jijini Dar Es Salaam na kuhitimu mwaka 2012. Mwaka huo huo wa 2012 alichaguliwa kujiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kusomea shahada ya sanaa ya Jiografia na elimu ya mazingira na kuhitimu mwaka 2015, pia ameandika kitabu kingine kiitwacho “CHANZO NI WEWE” na “WAKILIA TUTACHEKA”

Onesho la Kwanza

(Hali ya hewa ni ya baridi kiasi.  Upepo unavuma kwa kasi na kuifanya bahari ichafuke. Miti inayumba kulia na kushoto kufuata upepo, minazi nayo imetapakaa kila kona ya skuli inacheza sawa na mvumo wa upepo. Wanafunzi wanakimbizana huku na huko kila mmoja akiwa anawahi kurudi nyumbani. Kando ya barabara nje kidogo ya maeneo ya skuli, wanaonekana Mwanakombo, Mwanawima na Mwanaharusi wanaelekea kwenye kituo cha dala dala kurudi majumbani mwao.)

KONDA:                   (Konda anawazuia mlangoni) Wanafunzi mwisho

                                   watatu, wakusoma mnatoshaaa! Mnatoshaa hamsikii?

                                    Hili sio gari la watoto wa serikali bwana!

MWANAWIMA:     Heee, wee koma! Usinishike na mi – oili yako. Hujui  

                                    pesa ya sabuni inapotoka, hebu pisha huko! (Anatumia

                                    nguvu kuingia.)

KONDA:                    Kaa mbali, watu wako kazini, tusileteane uzuri hapa…

MWANAKOMBO:   Heee heee, halooooo, hiyo nayo kazi? Muda wote

                                     unanuka kwapa. (Abiria wanageuka na kumuangalia

                                     Mwanakombo.)

KONDA:                     (Anamkata jicho na kushindwa kujizuia, anamjibu)

                                      Kwako kazi nzuri ni zipi? Au ni zile za baba zenu

                                      kushinda majini kama vyura? (Abiria wote

                                      wanacheka.)

MWANAWIMA:        Kwenda mwana kwenda, uvuvi ndio shughuli kuu ya  

                                      uchumi hapa kisiwani wewe ulitaka awe anachungulia  

                                      kwenye mlango wa daladala kama wewe?

KONDA:                      Akalime karafuu anukie ili atoe shombo la samaki. Si

                                      wataka visivyonuka?

MWANAHARUSI:      (Anawanyamazisha wenzake) Hebu acheni kupayuka. Tumechoka na kelele tulikotoka. Tupumzisheni jamani.

DEREVA: (Anageuka nyuma) Oyaa usigombane na wa kusoma. Hao ndio matajiri wetu wa kesho. Angalia vichwa mwanangu siku mbaya hii.

KONDA: (Gari linaenda huku konda anaendelea kuita abiria) Haya

Stonetown kwa wajanja, wahi twendeee…

(Kadri gari lilivyozidi kwenda ndivyo abiria walivyozidi kushuka na kupungua. Mwisho wakabaki Mwanakombo, Mwanaharusi na Mwanawima.)

DEREVA: Mnaelekea wapi wasomi? (Anauliza huku akiwa anaangalia kwa kutumia kioo kilichopo mbele kabisa juu ya kiti chake.)

MWANAKOMBO: Stonetown (Anajibu kwa mkato.)

KONDA: Hee! Mnakaa Stonetown mnasoma Chukwani? Si mnapata usumbufu sana!

MWANAWIMA: Ndio maisha yetu haya, huu mwaka wa tatu tunakimbizana na daladala.

MWANAKOMBO: Matusi na kejeli za madereva na makondakta imekuwa sehemu ya maisha yetu, ndio maana hatuwashangai kwa maneno yenu ya  shombo na roho nyeusi kama zimekolezwa oili chafu. (Anaongea huku amebana pua) eti wa kusoma wametosha. (Anacheka kwa kejeli.)

DEREVA: Oyaaa, ongea na wadogo zako vizuri mwana uwasaidie, hawajakula hao. (Anamkonyeza konda kwa siri na kupeana ishara za Dole gumba.)

KONDA: Wagombanao ndio wapatanao, si unajua wanafunzi wakilegezewa

wanajaa! Usawa huu tutaishije kwa vijisenti vya wanafunzi? Unakuta gari

limejaa wanafunzi tu, ila msijali tuko pamoja.

MWANAKOMBO: Tumeshawazoea bana! Hata wasipojaa mna kasumba ya kutowapenda wanafunzi kisa wanalipa nusu nauli.

DEREVA: Hivyo hivyo, tuvumiliane warembo maana kwa upande wetu  ukiwa mpole tu unaharibu kazi.

MWANAHARUSI: Lakini kweli!

(Konda anakonyezana na dereva wake tena kisha anatoa simu yake ya mkononi na kumpa Mwanawima… bila kusema chochote.)

MWANAWIMA: Vipi? (Anamkodolea macho.)

KONDA: Namba yako ya simu basi!

MWANAWIMA: Heee! Hiyo simu umeninunulia mpaka unataka namba

                                 yangu? Mimi sina simu. (Anafunga ushungi wake vizuri.)

KONDA: Mmmm! Warembo kama ninyi mnakosaje simu? Yaani hata nokia ya tochi hamna?

MWANAWIMA: Hahaa, hatujaamua tu…

KONDA: Ulimwengu huu tulionao mtu hatakiwi kukosa simu. Mnakosa mambo mengi mazuri. Usijali kesho kuna simu ipo nyumbani haina kazi   nitakupatia.

DEREVA: Waambie watoto wazuri hakuna haja ya wao kuhangaika na usafiri tena, wameshakuwa rafiki zetu kila tukipita wakiliona gari letu wapande free.

MWANAKOMBO: Hapo mtakuwa mmetusaidia sana maana saa ya kurudi

tunapata shida haswaa! Tukipata hiyo simu tutakuwa tunawajulisha tulipo.

KONDA: Sawa, kesho saa kumi na mbili tutakuwa tumeshafika kituoni, mjitahidi kuwahi.

MWANAWIMA: Hahaa! Ila usumbufu hatutaki.

KONDA: Hamna usumbufu bwana, kwani nyie watoto?

DEREVA: (Anamwangalia Mwanaharusi huku akiwa anaendelea  

kuendesha gari) Mbona huyu mwingine haongei?

MWANAKOMBO: Huyo anaongea kama chiriku, haujamzoea tu.

MWANAHARUSI: Mimi simo kwenye mambo yenu, (Anamwambia kwa

Sauti ya chini…)

KONDA: Hakuna shida, hata peponi hawaingii watu wote…

MWANAWIMA: Huyo ndio kawaida yake ila anaongea sana tu. Inabidi    

umzoee tu.

Itaendelea………………………………………………………………….

Author: Gadi Solomon