Uundaji wa maneno ya Kiswahili

Amani Njoka-Swahili Hub

Lugha ya Kiswahili kama lugha nyingine duniani hupitia michato fulani mpaka sauti fulani zitokee kisha hizo sauti zikaunganishwa na kuwa maneno na baadaye lugha. Hata hivyo leo hivyo katika ukurasa huu hatutaangazia michakato ya uungaji wa sauti bali tutaangalia uundaji wa maneno ya lugha ya Kiswahili. Uundaji wa maneno ni moja ya mada zilizopo katika mtaala wa somo la Kiswahili kidato cha nne na hivyo kuwa moja ya mada yenye maswali hasa kipengele cha maswali ya insha.

Uundaji wa maneno, ni utaratibu wa kutengeneza maneno mapya ambayo hayapo katika lugha. Uundaji huu hutegemea michakato tofautitofauti aidha kwa kutumia maneno mapya au yaleyale yaliyopo. Ifuatayo ni michakato hiyo ya uundaji wa maneno katika lugha ya Kiswahili.

Kubadili mpangilio wa herufi: Neno hujengwa kwa mfuatano wa vitamkwa/sauti fulani. Mpangilio huunda neno lenye maana fulani. Hata hivyo, katika ,chakato wa kuunda neno jipya kwa kutumia njia hii, neno hilo hupanguliwa na kuunda neno/ maneno mengine yenye maana tofauti na lile la awali. Mfano ufuatao unaonesha baadhi ya maneno ambayo ambayo yakipanguliwa hubadili maana ya awali.

 1. Takataka linaweza kubadilika na kuwa: katakata
 2. Lima: imla, mali, lami, mila.
 3. Sikia: akisi, kiasi, kisia

Kuambatanisha maneno: Ni mchakato wa kuleta pamoja maneno mawili au zaidi ili kupata neno moja jipya lenye maana. Katika lugha ya Kiswahili kuna aina tatu za kuambatanisha meneno. Hata hivyo katika hatua hii tutaangalia aina za maneno zinazounda maneno mengine tu na sio aina za maneno yanayoundwa.

Njia ya kwanza ni kurudiarudia neno moja ili kupata neno lingine. Mfano; barabara, pigapiga, imbaimba nyumbanyumna, sawasawa n.k. Njia ya pili ni uungamishaji maneno mawili na kuendelea yenye hadhi tofauti, yaani kategoria tofauti. Mfano;

Nomino na Nomino

 • Askari+Kanzu= askarikanzu
 • Bwana + harusi=bwanaharusi
 • Mwana + jeshi= mwanajeshi
 • Afisa + Elimu=afisaelimu

Kufupisha maneno na kudondosha baadhi ya herufi/Akronimu: Mchakato huu ni uwekaji pamoja wa herufi za mwanzo za maneno mawili au zaidi au sehemu ya neno zima kudondoshwa na kubaki neno.

 • Baraza la Kiswahili Tanzania BAKITA
 • Chama Cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA
 • Chama cha Mapinduzi CCM
 • Tanzania Labour Party TLP

Ikumbukwe kuwa kuna aina zaidi ya moja za ufupishaji lakini katika mada hii tumezungumzia ufupishaji kwa ujumla.

Kutohoa: Ni usawazishaji wa maneno kutoka lugha nyingine ambayo huwa na matamshi au kuandikwa kwa namna inayofanana na ile ya lugha chanzo kwa kufuata sarufi ya lugha lengwa. Mfano, neno kama cigarette kutoka Kiingereza huwa na muundo na matamshi yasiyofanana na Kiswahili basi lilitoholewa sigara. Utohoaji hufanyika ili kupata msamiati utakaokidhi hutaji la lugha fulani kwa kuwa hakukuwa na msamiati unaokaribia kimaana au kumatamshi na huo ambao umetoholewa. Mifano zaidi imeoneshwa katika jedwali lifuatalo.

Kutoka NenoNeno la Kiswahili
Kiingereza shirt, lorry, carshati, lori, gari
Kireno mezimeza
Kihindi lakhilaki
Kisukuma ntemimtemi
Kihispania papayapapai
Kiarabushuktan, magharib, sadakshukrani, magharibi,sadaka

Uambishaji wa maneno: Uambishaji ni upachikaji au uongezaji wa viambajengo mwanzoni, katika na mwishoni mwa mzizi wa neno fulani ili kupata aina nyingine ya neno. Mara nyingi maneno haya hubadili kabisa kategoria. Mfano, m ikiambikwa mwanzoni mwa mzizi au shina cheza na ji kuambikwa mwishoni mwa shina hilo hubadili kategoria ya kitenzi cheza na kuwa nomino mchezaji. Maneno mengine ni:

 • Lima – mkulima
 • Piga – upigaji
 • shukuru-shukrani
 • Pika- mpishi.

Unyumbulishaji: Ni uwekaji wa viambajengo mwishoni mwa shima la neno ili kupata neno jipya bila kubadili maana ya msingi ya mzizi au shina hilo. Tofauti pekee ya unyumbulishaji na uambishaji kuwa; uambishaji unaweka huhusisha uwekezaji wa viambajengo mbele, katikati na nyuma wakati unyumbulishaji ni uwekaji wa viambajengo mwishoni tu. Mfano wa maneno ya unyumbulishaji:

 • Imba-imbia, imbiwa, imbiana, imbisha, imbishwa
 • Lima-limiwa, limia, limiana, limika
 • Tembea-tembelea, tembezwa, tembeleana.
 • Cheza-chezewa, chezea, chezesha, chezeana, chezeshea.

Aina hii ya uundaji wa maneno huenda sambamba na kauli za undendaji katika lugha ya Kiswahili.

Muigo/Tanakali sauti: Maneno kadha wa kadha katika lugha ya Kiswahili yametokana na jinsi au namna ambavyo sauti ya kitu, kiumbe au mnyama hutoa sauti yake. Vitun mbalimbali vya kutengenezwa au wanyama watoapo sauyti, watu huzukariri sauti na kuvipa majina ya sauti hizo vitu hivyo na hatimaye kuwa maneno mapya.

 • Pikipiki-hiki kifaa cha usafiri chenye magurudumu mawi;i kitumiacho moto na jina hili limetokana na mlio wake pik..pik..pik na wengine husema tuktuku.
 • Nyau/paka- ni kiumbe afugwaye mwenye kucha mithili ya chui au simba aliyepewa jina nyau kwa sababu ya mlio wake.
 • Bata-huyu ni ndege afugwaye (wakati mwingine hawafugwi) ambaye amepewa jina kutokana na anavyotoa kishindo akijisaidia, kula na kunywa maji.
 • Kengele-ni kifaa cha chuma kitoacho mlio fulani kikigongwa kwa ajili kuashiria jambo, tukio au wakati. Kifaa hiki hutoa sauti inayofanana na jina la kifaa hiki.

Maumbo na kazi ya vitu: Katika lugha ya Kiswahili kuna maneno ambayo yameundwa na kuitwa jina la kitu ambalo kwalo hunasibisha kitu hicho au kutoka na namna kilivyo. Mfano:

 • Kifaru-huyu ni mnyama wa porini, mwenye pembe mbili (kubwa na ndogo) juu ya kichwa chake, pembe hii huitwa kipusa. Umbo na tabia ya mnyama huyo ya kukimbia bila tahadhari, kupita kila mahali na vurugu kumesababisha gari la vita lenye kifaa cha kutolea milipuko kwa juu kama kipusa cha mnyama huyu huku likiwa na uwezo wa kupita popote kuitwa kifaru.
 • Kipimapembe- kifaa hiki kimepewa jina kutokana na kazi yake ya kupima pembe za maumbo mbalimbali.
 • Kipimajoto-kupima joto
 • Kidoletumbo-umbo kama kidole kidogo cha mwisho cha mkono.

Ama kwa hakika Kiswahili kimeundwa kwa maneno yaliyopatikana kwa namna mbalimbali, hii ni tabia ya lugha yoyote mathalani Kiingereza ambacho nacho limekopa maneno, kutohoa, kuunganisha na namna nyingine kama ilivyo Kiswahili. Hii ni tabia ya lugha zote.

Author: Gadi Solomon

2 thoughts on “Uundaji wa maneno ya Kiswahili

 1. kwa kweli nawapongeza kwa taarifa zenye ubora wa hali ya juu, mimi kama mdau wa kiswahili ninayesoma isimu ya kiswahili shahada ya awali UDOM, nafurahi mno kuona kiswahili sasa kinapewa kipaumbele. mimi pia mwenyekiti Chama cha wanafunzi (CHAWAKITA) tawi la UDOM najivunia sana kuwa mswahili, nasoma kiswahili na nakitangaza kiswahili . Nawaombeni mzidi kutuhabarisha zaidi Swahili hub.

  1. Asante sana kwa kutufuatilia. Endelea kukitangaza Kiswahili, kwa habari zozote na matukio ya Kiswahili usisite kutujulisha tuwajuze Wanakiswahili ulimwenguni. Swahili Hub ndicho chombo pekee kilichopo duniani kwa ajili ya habari zihusuzo lugha ya Kiswahili

Comments are closed.