Umuhimu wa Vitendawili vya Kiswahili

Amani Njoka, Swahili Hub

  1. Vitendawili huburudisha kwani hutegwa kwa njia ya uchangamfu na ushindani. Katika ushindani huo watu huweza kucheka na wakati mwingine kuchangamsha akili hasa hadhira inapokosa jibu.
  2. Huwaleta watu pamoja (huunganisha jamii) kwani vinapotegwa watu hukusanyika pamoja. Vilevile ili vitendawili vitegwe ni lazima kuwe na fanani na hadhira, hivyo watu hulazimika kukaa pamoja.
  3. Vitendawili hukuza uwezo wa kufikiria/kukumbuka kwani anayetoa jibu huhitajika kukumbuka jibu la kitendawili.
  4. Hukuza uhusiano baina ya vijana wanaochipukia na wazee wao kwani huwa ni moja ya njia bora ya wazee kuwausia vijana wadogo mathalani watoto.
  5. Vitendawili hutoa mafunzo kwa hadhira kwani huwa na maarifa ndani na jumbe mbalimbali.
  6. Vitendawili hukuza na kuhifadhi tamaduni kwa maana hupokezanwa kutoka kizazi hadi kizazi.
  7. Vilitumika kupitisha wakati na kuwafanya watoto wasilale mapema kabla ya chakula kuwa tayari.

Author: Amani Njoka