Waandishi waitwa kushiriki Tuzo ya Fasihi ya Afrika 2023

Mwandishi Wetu, SwahiliHub

Dar es Salaam. Waandaaji wa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika wametangaza wito kwa watu mbalimbali kuwasilisha miswada kwa ajili ya shindano la nane la tuzo hiyo, ambayo hapo awali iliitwa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika.

Kuanzia mwaka jana, jina hilo lilibadilishwa ili kuakisi jina la kampuni mama, ambayo ndiyo mdhamini mkuu, Safal Group Limited, kupitia kampuni zake tanzu za Mabati Rolling Mills (MRM) ya Kenya, na ALAF Limited ya Tanzania.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika ilianzishwa mwaka 2014 na Dk Lizzy Attree na Dk Mukoma wa Ngugi ili kutambua uandishi kwa lugha za Kiafrika na pia kuhimiza tafsiri baina ya lugha za Kiafrika.

Pia kutafsiri maandishi ya lugha nyengine kwa lugha za Kiafrika. Katika kipindi cha miaka yote hii, Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika pia imewasaidia waandishi walioshiriki katika mashindano ya Tuzo hii kwa maandishi yao kuchapishwa vitabu.

Wakati juhudi za kuhimiza kusoma na kuandika kwa Kiswahili zinaendelea, waandishi kutoka Afrika Mashariki na nchi nyengine za Afrika wamehimizwa kuwasilisha miswada yao na kushiriki katika shindano la mwaka huu.

Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika inauthamini uungwaji mkono mkubwa wa Safal Group katika kusaidia kuiendeleza Fasihi ya Afrika.

Katika mwezi wa Januari mwaka huu, washindi wa tuzo hii wa shindano la mwaka 2022 walitangazwa katika sherehe maalumu iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.

Wanaotaka kushiriki katika shindano la mwaka huu wanahimizwa kuiwasilisha miswada yao ambayo haijachapishwa, katika tanzu za riwaya, ushairi, mkusanyo wa hadithi fupi, wasifu na riwaya za picha. Vitabu vilivyokwisha chapishwa havitazingatiwa.

Zawadi za jumla ya Dola 15,000 za Marekani zitatolewa kwa mshindi wa kwanza katika utanzu wa riwaya na ushairi kila mmojawao atapata Dola 5,000; na washindi wa nafasi ya pili katika utanzu wa riwaya au ushairi, au utanzu wowote mwengine, watapata zawadi ya Dola 2,500 kila mmoja.

Miswada itakayoshinda itachapishwa vitabu na shirika la uchapishaji la Mkuki na Nyota Publishers (Tanzania), ambalo linaweza kushirikiana na wachapishaji wengine ili kurahisisha upatikanaji wa vitabu vilivyoshinda.

Vitabu vya miswada ya ushairi itakayoshinda vitafasiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund.

Sherehe ya kuwapa zawadi washindi wa mwaka 2023 itafanyika Januari 2024, na waandishi wote walioorodheshwa watahudhuria.

Author: Gadi Solomon