Waandishi watangaziwa fursa Tuzo za Mabati Cornell ya Fasihi 2021

 Gadi Solomon, Mwananchi

Waandaaji wa mashindano ya Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika yatakayofanyika kwa mara ya sita mwaka huu wamewataka waandishi mbalimbali wa vitabu kutuma miswada yao.

 Tuzo hii, iliyoanzishwa mwaka wa 2014 na Dk Lizzy Attree (Short Story Day Afrika) na Dk Mukoma wa Ngugi (Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani), ina madhumuni ya kuhimiza uandishi kwa lugha za Kiafrika, na kuhimiza sanaa ya tafsiri kutoka lugha za Kiafrika, baina ya lugha za Kiafrika, na kwa lugha za Kiafrika.

Baada ya kusimamisha Tuzo ya Mabati-Cornell mwaka 2020 kwa sababu ya janga la Covid-19, miswada iliyopelekwa mwaka jana pia itajumuishwa katika tuzo ya mwaka huu wa 2021.

Tuzo hiyo itatolewa kwa muswada bora ambao haujachapishwa, au kitabu kilichochapishwa katika miaka miwili kabla ya mwaka wa Tuzo katika tanzu za riwaya, ushairi, mkusanyo wa hadithi fupi, riwaya za picha na wasifu. Jumla ya $15,000 (za Marekani) zitatolewa kwa Mshindi wa Kwanza (riwaya)  – $5,000, Mshindi wa Kwanza (ushairi)  – $5,000, Mshindi wa Pili (katika utanzu wowote)  – $2,500 na Mshindi wa Tatu (katika utanzu wowote) – $2,500.

Mswada utakaoshinda utachapishwa kwa Kiswahili na mashirika ya uchapishaji ya Mkuki na Nyota Publishers (Tanzania) na East African Educational Publishers (Kenya).

Pia diwani bora itatafsiriwa kwa Kiingereza na kuchapishwa na Africa Poetry Book Fund. Sherehe ya kuwatuza washindi, itakayohudhuriwa na washindi wenyewe, itakuwa Afrika Mashariki.

Washiriki wanatakiwa kupeleka mswada au kitabu kilichochapishwa katika miaka miwili kabla mwaka wa Tuzo, hadi Mei 31, 2021.

Mwandishi mmoja anaweza kupeleka mswada mmoja tu au kitabu kimoja tu katika kila kipengele.  

Washindi hawaruhusiwi kushiriki kwa misimu miwili mfululizo tangu walipotangazwa kushinda.

Sehemu ya taarifa hiyo ilieleza mswada wa riwaya usipungue maneno 50,000 na wa ushairi usipungue kurasa 60 na kazi zote lazima ziwe za Kiswahili.

Author: Gadi Solomon