Wadau wa ushairi wamlilia Mzee Andanenga, azikwa Dar es Salaam

Tuzo Mapunda, Mwananchi
[email protected]

Dar es Salaam. Mwanasheria na mwandishi wa vitabu vya riwaya fasihi za Kiswahili na Kiingereza, Charles Mroka amemuelezea hayati Mzee Amir Andanenga kama mtu aliyekuwa na kipaji cha kutunga mashairi kwa kutumia mfumo wa uchapaji wa mtu asiyeona wakati wa uhai wake.

Mzee Andanenga aliyekuwa mwanafasihi nguli na mwasisi wa Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (Ukuta) alifariki usiku wa kuamkia jana Alhamisi Mei Mosi, akiwa kwenye Hospitali ya Dokta Mvungi Kinondoni alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na malazi yaliyokuwa yanamsibu.

Mroka aliyekuwa Mwandishi wa ansadi za Bunge la Tanzania kwa miaka 40, ametoa ushuhuda huo leo kwenye mazishi ya nguli huyo yaliyofanyika Makaburi ya Shamba Kinondoni.

Amesema Tanzania imepoteza mtu kwenye tasnia ya ushairi hasa kwenye ushairi wa kimapokeo na mtu aliyekuwa anafahamu historia ya washairi nchini.

“Andanenga ni kizazi kilichofanya Kazi na washairi nguli kama Marehemu Shaban Robert, Kanuta Abed, Saad Kandoro na wengine wengi alifanya kazi na vizazi vyote na alikuwa mshauri mzuri na hazina ya historia ya Kiswahili na ushairi,” amesema.

“Kuna kitu ningependa kukisema katika nchi yetu ebu tuwazike wasanii wetu wakiwa haki tusiwazike wakiwa wamekufa nina maana kama nisifa au tuzo tuwape wakiwa hai wajisikie ni upungufu ulipo kwetu Sana,” amesema.

“Andanenga ni mtu aliyependa ushairi, Kiswahili na wakati wote ukimtembelea nyumbani hata kama unahitaji kumbukumbu ya ushairi fulani mbali na kwamba alikuwa haoni lakini alikuwa na uwezo wa kukupatia bila kusaidiwa na mtu,” amesema.

Mroki aliyeandika diwani ya Mroki amesema, Andanenga kabla ya kuwa mshairi alikuwa mfanyakazi wa Serikali na alikuwa anafanya kazi Ofisi za Bunge la Tanzania akiwa kama karani na baadaye kuhamishiwa katika Wizara ya Maji,”amesema

Amesema ilipofika mwaka 1972 alipata maradhi ya macho na alikwenda kufanyiwa operesheni Hospitali ya Taifa Muhimbili akiwa katika hatua hiyo bahati iliyokuwa mbaya macho yake yalipoteza nguvu kabisa ya kuona.

“Licha ya kwamba lengo la operesheni ile ulikuwa nzuri lakini ilisababisha asione tena. Ingawa hali hiyo haikumkatisha tamaa baada ya kupovuka macho alianza kutumia mfumo wa uchapaji wa mtu asiyeona,” amesema.

Amesema aliendelea kuchapa kazi zake kwa mfumo huo na alitoa diwani mbalimbali ikiwemo diwani ya Ustadhi na nyingine ambazo hazijaingizwa kwenye mfumo mtandao.

“Diwani ya Ustadhi iliendelea kukaa na alikuwa anapigania zitumike kwenye taasisi za elimu kuwaomba watumie kwenye mtalaa ndipo Mwaka 1998 iliteuliwa kuwa kitabu cha kiada kwa wanafunzi wa sekondari fasihi ya Kiswahili mashairi,” amesema.

Amesema hata hivyo nguli huyo aliyewahi kutunukiwa tuzo sufufu za lugha ya Kiswahili kutokana na ubora wake wa kutunga aliendelea kutunga vitabu vingine kama bahari ya elimu ya ushairi na vilitumika mataifa mbalimbali ikiwemo Rwanda na Kenya.

“Ukiacha Kazi yake ya ushairi Andanenga alikuwa mtu anayeibua maswali na misamiati mbalimbali mfano kuna neno ‘bahati mbaya’ alikuwa anakataa bahati ni kitu kizuri utasemaje kitu kizuri kiwe bahati mbaya ni vizuri kuita isivyo bahati badala la kusema bahati mbaya,” amesema

Amesema alikuwa mzee wa kuzua mjadala ingawa alikuwa anakusanya wafuasi wengi ambao wanasema isivyo bahati ingawaje kuna wanazuoni wengine wanampinga.

“Andanenga alisoma hadi darasa la nane mkoa wa Ruvuma ingawaje hakuendelea kutokana na sababu za kiuchumi,” amesema.

Kwa upande wake Jumanne Undi aliyekuwa rafiki yake wa karibu amesema Mzee Andanenga alizaliwa Kilwa Mkoa Lindi mwaka 1936 amefariki akiwa na miaka 88.

Amesema mashairi mengi aliyoandika yalikuwa yanavutia, yakagusa maisha ya watu moja kwa moja. Lakini yalijaa utajiri mkubwa wa lugha, nahau, methali na vibwagizo vingi. Yalisaidiakukuza lugha adhimu ya Kiswahili, kiasi kwamba yaliitangaza nchi yetu kwa mapana makubwa.

Kutokana na utajiri huo, vitabu vingi alivyotunga mashairi na hata wale walioandika katika magazeti, vilitumiwa kufundishia katika shule za msingi na sekondari, na baadhi yake vilitumiwa kwa kiwango kikubwa katika vyuo vya elimu ya juu.

“Kwa bahati mbaya, umahiri na ushindani wa watunga mashairi ulianza kufifia miaka ya tisini, na tangu wakati huo hadi sasa ni watunzi wachache sana waliobaki, na hata wao hawatungi tena yenye mguso na hisia kubwa kama walivyokuwa watunzi wa zamani.,” amesema Undi.

Author: Gadi Solomon