Wako wapi


Wawapi wale manamba, walio watapitapi,
Walo jisifu kuimba, uimbi wao ukupi,
Kwa mbwembwe walijigamba, Kwa hojo zilo makapi,
Kunuka wala hukwepi, sana sana ukichamba.

Sana sana ukichamba, harufu mbi huchupi,
Izara itakubamba, kama mvukwa na chupi,
Nawauzani wajomba, tambo zenu ziko wapi,
Kunuka wala hukwepi, sana sana ukichamba,

Mlo kigonga usumba, kwa jina hili mvipi,
Urongo mliupamba, tusijue kweli ipi,
Cha Siyu kimewakumba, kimbunga ama ni vipi,
Kunuka wala hukwepi, sana sana ukichamba,

Mambo hayendi kimwamba, hadaa zatoka wapi,
Kivambo kimewavamba, ja mwana mpokwa pipi,
Mayi huwasoza mamba, seuze ninyi wa pupi,
Kunuka wala hakwepi, sana sana ukichamba,

Tama navua kiremba, na sefu yangu situpi,
Kila mchezea simba, maisha huwa mafupi,
Tambeni mlivyo tamba, yeo tujue mkupi,
Kunuka wala hakwepi, sana sana ukichamba.
MKANYAJI
Hamis AS. Kisamvu
Baitu shi’ri
kissamvujr@gmail.com
255715311590
Mabibo- Dar es salaam
TANZANIA

Author: Gadi Solomon