Wahitimu 35 watunukiwa shahada ya Kiswahili UDSM, mwanafunzi wa Kiswahili aongoza

Amani Njoka, Swahili Hub

Kwa ufupi: Walitunukiwa digrii hizo huku wakila kiapo kuwa watayatendea haki maarifa waliyoyapata hususani ya lugha ya Kiswahili. Vilevile katika mahafali hayo HappyLight Joseph alitangazwa kuwa mwanafunzi bora kwa ngazi ya shahada ya awali kwa chuo kizima.

Da es Salaam. Jumatano, tarehe 20 Novemba 2019 ilikuwa siku muhimu na yenye furaha kubwa kufuatia mahafali ya shahada za awali zinazotolewa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Zaidi ya wahitimu 3,000 walihitimu ngazi ya cheti, stashahada na shahada katika fani mbalimbali.

Miongoni mwa wahitimu waliotunukiwa tuzo hizo katika mahafali ya jana ni pamoja na wanafunzi takribani wanafunzi 35 waliohitimu mafunzo yao ya shahada ya awali ya elimu ya jamii katika Kiswahili. Sambamba na kunukiwa tuzo hizo, wahitimu hao waliahidi kuyatumia vyema maarifa waliyopata katika elimu ya Kiswahili kwa taifa na nje ya mipaka yake.

Akizungumzia mahafali hayo, mmoja wa wahitimu wa shahada ya awali katika Kiswahili, Gabriel Mwabupina alisema kuhitimu kwao sio bahati mbaya bali ni makusudi maalum ya Mwenyezi Mungu na kuwawezesha kupata maarifa hayo na hivyo jamii ijiandae kuyapokea mabadiliko kupitia hicho alichojifunza.

“Kama mtaalamu wa lugha ya Kiswahili, nitatumia maarifa niliyoyapata kuandika na kusema ili kuujulisha ulimwengu kuwa lugha ya Kiswahili ni bora na ina mchango mkubwa katika maendeleo na hivyo ulimwengu unapaswa kuitambua lugha hii.”

Mhitimu mwingine Hasheem Juma alisema anamshukuru Mungu aliyemwezesha kuhitimu shahada hiyo na ni hatua nzuri ya kuridhisha kwake. Pia, aliiomba serikali iweke sera madhubuti zitakazowatambua wataalamu wa Kiswahili kwani wanahitimu wengi lakini hakuna mazingira mazuri kwao ya kukiuza Kiswahili licha ya ahadi nyingi za serikali.

“Elimu yangu itanisaidia kueneza Kiswahili Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla,” alisema Juma.

Aliongeza kuwa, “Serikali iweke wazi sera zitakazowawezesha wataalamu wa Kiswahili kupata fursa zaidi ya kukiuza Kiswahili ndani na nje ya nchi kwani fursa ni nyingi lakini mazingira ya wao kuwa katika soko la ajira bado si mazuri na hivyo kusababisha wahitimu wengi kubaki mitaani.”

“Ninaiomba serikali iweke utaratibu na mikakati itakayotuwezesha kufika ulimwenguni kukitangaza Kiswahili ili taifa lifaidike pamoja na sisi pia.” Aliongeza.

Mwanafunzi HappyLight Joseph aliyeongoza kwa kupata wakia (GPA) wa juu wa 4.8, akihutubia wahitimu wenzake na wageni waliohudhuria mahafali hayo mbele ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alisema ni furaha na anamshuru kwa kumfanikisha na kwamba atayatumia maarifa aliyoyapata kukikuza Kiswahili.

“Ninahisi furaha sana na namshukuru Mungu. Maarifa niliyoyapata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndani na nje ya darasa nitayatumia kwanza kukuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania na zaidi kuwa balozi mzuri wa chuo katika kupambana na changamoto hasa katika sekta ya elimu,” alisema.

HappyLight ambaye ni mhitimu wa shahada ya awali ya Kiswahili katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ametunukiwa tuzo ya kuwa mwanafunzi bora wa chuo katika ngazi ya awali kwa ufaulu wa juu kwa kupata wakia (G.P.A) wa 4.8.

Tarehe 20 Novemba 2019 ilikuwa ni kilele cha mahafali ya 49 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho na wanafunzi mbalimbali walitunukiwa shahada katika ngazi mbalimbali, stashahada pamoja vyeti.

Author:

2 thoughts on “Wahitimu 35 watunukiwa shahada ya Kiswahili UDSM, mwanafunzi wa Kiswahili aongoza

Comments are closed.