Wanafunzi shahada ya Kiswahili wafunguka

Nabil Mahamudu na Loveness John

Dar es Salaam. Wanafunzi wanaosoma kozi mbalimbali za lugha ya Kiswahili wamezungumza kwa njia ya simu wakielezea changamoto na fursa wanazokutana nazo katika uga huo katika maeneo mbalimbali wanakofanya mafunzo kwa vitendo hapa nchini.

Taaluma ya lugha ya Kiswahili imejikita katika utoaji wa kozi za ualimu wa Kiswahili kwa wageni, uhariri, tafsiri na ufasiri, ukalimani na uhakiki wa lugha.

Baadhi ya wanafunzi hao wamesema wamebaini changamoto na fursa wakiwa katika vituo vyao vya mafunzo kwa vitendo.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya Kiswahili, Paschalina Katoto ambaye anafanya mafunzo kwa vitendo  Baraza la Kiswahili Zanzibar (Bakiza) kitengo cha Uhariri, amesema baadhi ya msamiati inayotumika Zanzibar ina utofauti na ile ya Bara katika matumizi.

Katoto amesema changamoto hiyo inawakabili na wanafunzi wenzake ambao wametoka katika vyuo vya Tanzania Bara, huku akitoa mfano wa maneno  kama vile Mfereji – Bomba, Skuli – Shule, Ukumbini – Sebureni.

Mwanafunzi mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya awali Fabian Letema amesema changamoto ambayo amekumbana nayo ni kufanya mafunzo katika taaluma ambayo hajaisomea ya utangazaji redioni. Hivyo imeletea ugumu katika utendaji wa kazi.

 Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gladness Payovela amesema changamoto ambayo anaona ni suala la fedha, wanafunzi wanaochukua Shahada ya Kiswahili katika ngazi ya awali hawapokei fedha za mafunzo kwa vitendo.

“Kuna baadhi ya vituo vya Kiswahili kwa wageni vipo mbali hivyo wanafunzi wanashindwa kuomba kufanya  kazi ili kupata uzoefu kwa sababu ya kukosa fedha,” amesema Payovela.

 Mwanafunzi wa Shaada ya awali wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Moses Cliff  amesema changamoto anayokumbana nayo ni uchache wa vifaa vya kufanyia kazi, kwa sababu kazi ya uhariri, tafsiri, na ikisiri ni kazi ambazo zinategemea vifaa vya kieletroniki.

Irene Mhandisa mwanafunzi wa Shahada ya awali ya Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema katika kituo chake alichopangiwa kufanya mafunzo kwa vitendo kuna uhaba wa kazi ukilinganisha na taaluma za lugha ya Kiswahili alizojifunza.

 Mhandisa amesema vitu anavyokutana navyo katika mazingira halisi ni tofauti na vitu alivyojifunza darasani. Hivyo inamsababishia ugumu katika kuzoea na kujifunza.

Rukia Ramadhani mwanafunzi wa Shahada ya awali katika Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema changamoto anayokumbana nayo ni vifupisho vya vyeo mbalimbali ambavyo vimetokana na lugha ya kigeni: Mfano Afisa utumishi wilaya (DHRO), Mwekahazina Wilaya (DT), Mkaguzi wa ndani (DIA), Mganga mkuu wa wilaya(DMO), Mkuu wa wilaya (DC), Timu ya Usimamizi ya Halmashauri (CMT).

Nabil Mahamudu mwanafunzi wa Shahada ya awali ya Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, changamoto kubwa anayokumbana nayo ni ufuataji wa mwongozo wa uandishi.

“Uandishi tuliouzoea chuoni ni tofauti na uandishi wa taasisi kama chombo cha habari ambako kuna mtindo wa upekee,” amesema.

Author: Gadi Solomon