Dar es Salaam. Wanafunzi watatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wanaosoma Kiswahili wamepatiwa udhamini wa masomo hayo ikiwa ni sehemu ya kuiunga mkono Serikali katika kukuza lugha hiyo.
Wanafunzi walionufaika na ufadhili huo mwaka huu kwa kudhaminiwa na Kampuni ya Alaf Limited ni Issa Makoye, Juditha Mwilolezi na Violeth Obimbo ambao kila mmoja anapokea zaidi ya Sh2.93 milioni.
Akizungumza leo Alhamisi Desemba 21, 2023 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kukabidhi hundi kwa wanafunzi hao, Meneja Masoko wa Alaf, Isamba Kasaka amesema: “UDSM mmetupa ushirikiano mkubwa katika zoezi hili la kuwadhamini wanafunzi na inatupa moyo wa kuendelea kuwadhamini wanafunzi kila mwaka.”
Kasaka amesema wanafunzi wanaosoma Kiswahili katika chuo hicho wanafadhiliwa kwa mara ya tano mfulululizo sasa.
“Huu ni mwaka wetu wa tano mfulululizo kutoa udhamini kwa wanafunzi wa UDSM kama njia ya kukuza lugha ya Kiswahili,” amesema Kasaka.
Amesema kampuni hiyo imekuwa ikifanya hivyo kupitia Alaf Foundation kwa kuzingatia umuhimu wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.
Pia, amesema kampuni hiyo imekuwa ikijihusisha na utoaji wa Tuzo za Fasihi ya Kiswahili na imekuwa mdau muhimu katika mchakato wa utoaji wa tuzo hizo.
“Jambo hili pamoja na mambo mengine limelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha kuwa, tunakitangaza Kiswahili ndani na nje ya nchi kwa kuwa lugha hii ni miongoni mwa tunu za Taifa letu na urithi wa pekee tulioachiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere,” amesema Kasaka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Udhibiti Ubora wa UDSM, Profesa Pendo Malangwa ameishukuru Alaf kwa jitihada zake za kukuza Kiswahili.
Hata hivyo, amewataka wanafunzi hao watumie udhamini huo vizuri ili wawe bora zaidi katika matumizi ya lugha hiyo.
Profesa Malangwa amesema tangu kuanzishwa kwa ufadhili huo, tayari wanafunzi 15 wameshanufaika na baadhi yao wamefanikiwa kupata ajira sehemu mbalimbali ikiwamo UDSM.
Maoni Mapya