Wasanii watakiwa kutumia Kiswahili fasaha

Wasanii wa filamu nchini wameshauriwa kuandaa kazi zenye maudhui ya kiasili na kutumia lugha ya Kiswahili fasaha ili kuendelea kutangaza lugha hiyo kimataifa na kuvitangaza vivutio vilivyopo Tanzania.

Akizungumza na wadau wa sanaa nchini wiki hii Mei 21, 2024 wakati wa uzinduzi wa chaneli mpya yenye maudhui ya filamu, katuni kwa watoto ‘Swahili Plus’, mwakilishi kutoka, Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) Edward Nnko amesema anatambua mchango mkubwa unaofanywa na kazi za filamu nchini katika kutangaza lugha ya Kiswahili na kukipa thamani zaidi kwani kupitia kazi hizo mataifa mengine wamekuwa wakifatilia.

“Wasanii mna mchango mkubwa katika kuendeleza lugha ya Kiswahili kimataifa na kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo nchini, na hili linawezekana iwapo mtazingatia matumizi ya Kiswahili sanifu katika kazi zenu za sanaa,” amesema.

Meneja Masoko wa Kampuni ya Startimes, David Malisa ameeleza kuwa wamekuwa wakitoa vipindi mbalimbali vyenye maudhui tofauti tofauti hivyo kwa sasa wamezindua chaneli mpya ambayo itawapa fursa zaidi wasanii wa Kitanzania kuonekana.

Aidha amesema filamu zaidi ya 120 zitaonekana kupitia St Swahili Plus ambapo filamu hizo hazijawahi kuonekana popote pale zikiwa zimesheheni sura mpya za wasanii wachanga.

Msanii wa Filamu nchini Daudi Michael maarufu ‘Duma ‘ amewapongeza wadau hao wa sanaa kwa kuona ipo fursa ya kuwa wadau wakubwa wa kazi za sanaa na kutengeneza daraja la wasanii kufanya vizuri na kutengeneza kazi zenye viwango na shindani.

Author: Gadi Solomon