
Juma Issihaka, Mwananchi
Dar es Salaam. Washindi mbalimbali wamezawadiwa tuzo ya Taifa za Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu zilizoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), huku mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi, Peter Elias akiibukia nafasi ya nne kwa upande wa mashairi akipata zawadi ya cheti.
Katika kundi hilo, aliyeshinda ni Amri Abdalla na kupata zawadi ya fedha Sh10 milioni, huku Shaaban Athuman Maulid akiwa nafasi ya pili akipata Sh7 milioni na wa tatu ni Suphian Almas aliyepata Sh5 milioni.
Kwa upande wa riwaya aliyeshinda ni Hamis Kitare (Sh10 milioni), nafasi ya pili ni Nickson Damas (Sh7 milioni), wa tatu ni Zainab Ali (Sh5 milioni).
Miongoni mwa wageni waliohuhuria utoaji wa tuzo hizo ni, Profesa Kitila Mkumbo ambaye amehimiza utamaduni wa kusoma vitabu.
Amesema kusoma zaidi vitabu kunakufanya uwe mgumu wa kukasirika haraka pale unapopatwa na maudhi.
Kwa mujibu wa Mtaalamu wa Saikolojia ya Elimu na Mafunzo ya Mitalaa, Profesa Mkumbo anayesoma vitabu aghalabu huwa na maarifa lukuki.
“Utafiti wa baiolojia unaonyesha watu wanaoishi sana ni wale wenye tabia ya kusoma zaidi.
“Mimi tangu nimfahamu Profesa Issa Shivji Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1995 hadi leo yupo hivi hivi, vivyo hivyo kwa Mwalimu Mabala (Richard) kwa sababu wanasoma sana,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, hata anayesumbuliwa na msongo wa mawazo, kusoma hasa vitabu vya hadithi ndiyo tiba yake.
Amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa anayesoma vitabu zaidi si rahisi kukasirika haraka na kusisitiza jamii isiyosoma kiakili huwa na changamoto.
Alipoulizwa idadi ya vitabu alivyosoma hadi sasa, Profesa Shivji amesema ni vigumu kukumbuka, lakini amekuwa akisoma vitabu viwili vyenye kurasa kati ya 200 hadi 300 kila wiki mbili.
“Siwezi kusema vingi kwa sababu kuna vitabu vingi vya kusoma, mimi pia nimeandika vitabu kama 20 na kuhariri kama saba hivi,” amesema Profesa Shivji ambaye pia ni mtaalamu wa sheria.
Kwa upande wa Mwalimu Mabala amesema hadi sasa ni maelfu ya vitabu ameshasoma, ingawa ni vigumu kutaja idadi kamili.
“Mimi ni mwalimu wa fasihi raha yangu ni kusoma vitabu, nimehariri vingi na kutafsiri pia,” amesema.
Amebainisha amekuwa akisoma vitabu kwa kipindi cha miaka 60, akikadiria zaidi ya 1,000 alivyosoma hadi sasa, huku akiandika riwaya mbili, vitabu vya watoto zaidi ya 20 na mafunzo 15.
Maoni Mapya