Watanzania wanne wang’ara Tuzo za Fasihi, wazoa mamilioni

Nairobi. Watanzania wanne wameng’ara kwenye mashindano ya Tuzo ya Fasihi ya Safal-Cornell kwa mwaka 2023, kwa kuibuka washindi kwenye vipengele vya riwaya na ushairi kwenye mashindano, yaliyofanyika Ijumaa Februari 11, 2024 jijini Nairobi, huku wakiwabwaga washindani wao Wakenya.

Mwandaaji wa mashindano hayo Profesa Mukoma wa Ngugi, ambaye ni mtoto wa mwandishi maarufu wa vitabu, Prof Ngugi wa Thiong’o, kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani, anakosoma fasihi amewapongeza washiriki wote kwa kutuma kazi zao ili zishindanishwe.

Mashindano hayo huwa huandaliwa kila mwaka, chini ya ufadhili wa Safal Group, kupitia kampuni yake ya Mabati Rolling Mills, inayotengeneza mabati nchini Kenya.

Kutokana na matokeo yaliyotangazwa na majaji Ijumaa, waandishi Philipo Oyaro na Ahmad Simba kutoka Tanzania waliibuka washindi kwenye kipengele cha riwaya.

Wawili hao walishinda kupitia vitabu vyao ‘Dunia Duara’ na ‘Safari ya Maisha’ mtawalia. Wawili hao ndio walikuwa wakiwania tuzo katika kipengele hicho, pamoja na mwandishi Nicholas Ogal kutoka Kenya, kupitia kitabu chake ‘Salome Anaishi’.

Watanzania wengine waliong’aa katika kipengele cha ushairi, ni Fatuma Salim na Lenard Mtesigwa kuibuka washindi. Walishinda kupitia madiwani yao ‘Changa la Macho’ na ‘Ndani ya Subira Kichwangomba’.

Mkenya wa pekee aliyekuwa akiwania tuzo katika kipengele hicho ni John Karithi kupitia diwani yake ‘Ushairi wa Maisha ya Kesho.’

Akiwatangaza washindi, Profesa Kyallo Wamitila aliyekuwa Jaji Mkuu alisema kuwa jumla ya miswada 196 iliwasilishwa kwa jopo la majaji.

Alisema kuwa kila mmoja ni mshindi, kwani miswada yote ilikuwa na ubora wake.

“Miswada yote ilikuwa na ubora wake, japo lazima tungeiteua miswada bora zaidi,” akasema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Simamizi ya Tuzo hizo, mshairi wa Kiswahili, Abdilatif Abdallah, alisema kuwa msukumo mkubwa wa tuzo hizo ni kuwapa nafasi Waafrika kuandaa tuzo zao wenyewe ili kuendeleza lugha asilia.

Mshindi katika vipengele vyote viwili (riwaya na ushairi) huzawadiwa Sh12.4 milioni huku mshindi wa pili akinyakua Sh6.2 milioni katika kipengele chochote kile.

Author: Gadi Solomon