Watanzania wanyakua Sh28.8 mil Tuzo za Kiswahili Kenya

Amani Njoka na Gadi Solomon, Swahili Hub

Kwa ufupi: Watanzania watatu wameibuka washindi wa Tuzo za Fasihi ya Kiswahili za Mabati-Cornell kwa mwaka 2019 ambazo zimefanyika nchini Kenya kwa mwaka huu. Hafla ya ugawaji wa tuzo hizo kwa mwaka 2018 ilifanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka jana.

Nairobi. Watanzania watatu wamejishindia zawadi za jumla ya Dola 12,500 ambazo ni sawa na  Sh28,850,000 milioni baada ya kuibuka washindi kwenye Tuzo za Fasihi ya Kiswahili za Mabati Cornell zilizofanyika jana Alhamisi kwenye Hoteli ya Intercontinental Nairobi nchini Kenya.

Akitangaza washindi wa tuzo hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Safal Group, Anders Lindgren na Mwenyekiti wa Bodi ya Tuzo ya Kiswahili, Abdilatif Abdalla waliwataja washindi hao ambao ni Lello Mmassy ambaye ni mwandishi wa riwaya na Moh’d Khamisi Songoro mwandishi wa mashairi ambao ni kutoka Tanzania waliopokea dola za Marekani 5,000 kila mmoja.

Mtanzania mwingine alishika nafasi ya pili ni Rashid Ali na kujinyakulia dola za Marekani 2,500 za Marekani huku Mkenya John Wanyonyi naye alipata zawadi ya Dola 2,500.

Mwandishi Mmasi amejipatia tuzo kupitia kitabu chake cha riwaya, Mimi na Rais, Moh’d Khamisi Songoro amepata tuzo hiyo kupitia ushairi, Diwani ya Nusu ya Moyo na Rashid Othman Ali, alinyakua tuzo yake ya mshindi wa pili katika ushairi kupitia, Diwani ya Mji wa Kambare.

Akizungumza baada ya kupata tuzo hiyo, Mmasi aliwashukuru waandaaji na majaji kupitia ukurasa wake wa Twitter kwa kupata nafasi hiyo aliyoibuka mshindi wa kwanza kwenye kipengele cha uandishi wa riwaya.

“Mke wangu amekuwa sehemu muhimu katika safari yangu ya uandishi. Yeye ndiye aliyegharamia uchapaji wa nakala za mwanzo za Kitabu cha Mimi na Rais,” alisema Mmassy.

Naye Songoro alisema watunzi wengine wasikate taamaa na waaendelee kuandika na ksuhiriki mashindano hayo.

“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha nishinde tuzo hii. Nawashauri watunzi wengine wasikate tamaa, waendelee kupambana na wanawaza kushinda na wao,” alisema Songoro.

Mwandishi maarufu wa Vitabu nchini Tanzania, Richard Mabala aliwapongeza washindi wa tuzo hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema, “Hongereni sana washindi. Hongereni sana MabatiCornell kwa kuendelea kuwezesha fasihi ya Kiswahili kupitia kwa tuzo hili.”

Tuzo hizo zimeandaliwa na Safari Group, Aluminium Africa Limited (ALAF), Mabati Rolling Mills Limited (MRM) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Cornell cha nchini Marekani.

Author: Gadi Solomon