Waziri Bashungwa azindua vifa vya ukalimani

Gadi Solomon, Swahilihub

gslomon@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imenunua vifaa vya ukalimani vyenye thamani ya Sh187.5 milioni ambavyo vitasaidia kuimarisha taaluma na wakalimani nchini.
Akizungumza kwenye sherehe ya uzinduzi iliyofanyika kwenye viwanja vya Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) mwishoni mwa wiki, Waziri Innocent Bashungwa alisema vifaa hivyo vimenunuliwa ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa serikali katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.
Alisema Bakita inatakiwa kuendelea kukibidhaisha Kiswahili ili kuendana na Kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kuanzia sasa baada ya uzinduzi, tutaanza kufanya kikao kila mwezi ili kufanya ufuatiliaji wa vipaombele tulivyojiwekea,” alisema Waziri Bashungwa.
Alisisita Bakita kuanza kutumia vifaa hivyo ili kuandaa wakalimani ambao watatumika kwenye mikutano ya kitaifa na kimataifa.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pauline Gekul alisema baraza hilo linatakiwa kwenda na kasi ili kuwahudumia wananchi na wageni wanaohitaji huduma zake.


Alisema kasi ya kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali zinazotumika na wizara hairidhishi.
“Kama kuna uhaba wa wafanyakazi, baraza liwasiliane na wizara kwasababu kazi ya kutafsiri sheria na kanuni mbalimbali za wizara bado ni ndogo,” alisema Naibu waziri Gekul.


Mkurugenzi wa Utamaduni, Dk Emmanuel Temu alilipongeza baraza hilo kuendeleza ushirikiano na Baraza la Kiswahili Zanzibar(Bakiza) katika utendaji wa shughuli zake.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Bakita, Consolata Mushi amesema vifaa vilivyonunuliwa vitatumika kuwapima wakalimani nchi nzima ili wale watakaokidhi vigezo watumike kwenye mikutano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.


Amesema pia vifaa hivyo vitatumiwa na vyuo vikuu vinavyofundisha kozi ya ukalimani kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.
Alisema ni vyema Bunge la Afrika Mashariki kuanza kutumia lugha ya Kiswahili kwenye vikao vyake ili kupanua wigo wa fursa za ukalimani.

Author: Gadi Solomon