Waziri Dk Chana kuongoza Kongamano la Kiswahili Mwanza

Saada Amir, Mwananchi

Mwanza. Zaidi ya washiriki 150 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajia kukutana jijini Mwanza kwenye kongamano la kimataifa la kujadili hali ya Kiswahili na mustakabadhi wake kwa maendeleo ya jamii na Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Agosti 7, 2023, Mwenyekiti wa Chama cha Lugha na Fasihi ya Kiswahili Tanzania (Chalufakita), Dk Mussa Hans amesema kongamano hilo litaongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana Agosti 9 na 10, 2023 katika hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza.

“Mada kuu ya kongamano mwaka huu ni Nafasi ya Kiswahili Kitaifa na Kimataifa na litahudhuriwa na mabalozi takribani 15 wanaoiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali, baadhi watahudhuria ana kwa ana na wengine watashiriki kwa njia ya mtandao,” amesema

Mhariri Msaidizi wa Chalufakita, Dk Issaya Lupogo amesema kongamano hilo litahusisha uwasilishaji wa makala mbalimbali ikiwemo ya kuangazia uga wa Kiswahili na Tehama, kutakuwa na baraza la waswahili pamoja na upimaji afya bure.

Mwenezi wa chama hicho, Flora Mallema amesema kongamano hilo litapambwa na usiku wa mswahili ambao utahusisha burudani mbalimbali za Kiswahili, utamaduni wa mswahili kama vile ngoma za asili, tenzi, miziki ya kisasa yenye asili ya kiafrika na kitanzania.

“Baada ya kumaliza mawasilisho hayo tutakuwa na ziara ya kitalii, jiji letu la Mwanza lina vivutio vingi vya utalii kwa hivyo wageni na wadau watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vilivyopo jijini Mwanza,” amesema Athumani Salum, ambaye ni Katibu Mkuu Chalufakita

Author: Gadi Solomon