Waziri Mkuu asisitiza kuenzi lugha ya Kiswahili

Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuienzi na kuitumia lugha ya Kiswahili kwani ndiyo lugha iliyotumika na waasisi wetu wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.

Waziri Mkuu aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa Kongamano la Kutambua na Kuenzi Mchango Anuwai wa Historia ya Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam.

“Ni lazima kila mmoja wetu ajivunie na kuienzi lugha yetu adhimu ya Kiswahili kwani ndiyo lugha iliyotumiwa na viongozi wetu wakati wa harakati za ukombozi wa Bara letu la Afrika,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

“Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ihakikishe inayalinda maeneo yote yaliyotumika katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika hapa nchini,” Majaliwa.

“Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ihakikishe inakusanya nyaraka, mali na vifaa vyote vilivyotumika wakati wa harakati ya ukombozi wa Bara la Afrika ili viweze kuhifadhiwa kwenye makumbusho ya Taifa kwa ajili ya kulinda historia ya ukombozi kwa matumizi ya vizazi vijavyo,” alisema Waziri Mkuu.

Aliongeza kuwa, ” Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii mshirikiane kuyatambua maeneo yote yaliyotumika kwenye harakati za ukombozi ili kuyalinda na yatumike kwa ajili ya utalii wa Kihistoria.”

Kongamano hilo lililofunguliwa 21 Mei, 2021 lilifanyika kwa siku tatu ambapo lilijumuisha mijadala pamoja na kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo nchini.

Author: Gadi Solomon