Wosia kwa wajukuu

 Na Jacob Qorro

(SEHEMU YA KWANZA)

Mara baada ya kupata uhuru Mwalimu  Nyerere aliiweka Tanzania katika reli ya kuwa taifa lenye uhuru wa kweli baada ya kutawaliwa na wakoloni kwa miaka arobaini. Kwa maana nyingine alitaka Tanzania iwe nchi inayojitegemea kama wakoloni walivyoikuta kwani wakoloni hawakuwakuta akina Mkwawa na Isike wala Mirambo  ombaomba na alitaka  tuishi katika utamaduni wa kiafrika wa ujamaa kwani taifa au kabila lisilothamini utamaduni na mila zake kwa maneno ya Nyerere ni Taifa au kabila mfu yaani iliyokufa ingawa watu wake wanaweza kuwa hai.

Baada ya Mwalimu  kustaafu waliomfuata badala ya kuiwekea reli hiyo aliyoisanifu Nyerere katika kiwango cha juu cha  ‘standard gauge’ ni kama waliirejesha tenaTanzania  kwa wakoloni waliotutawala na hata wale wasiotutawala yaani wakoloni wapya. Kama Taifa tuliteleza nyuma kijumla yaani yale mema yote ya Nyerere tuliyaona dhambi na hakuna aliyekemea ufidhuli huo,na madhaifu yake tukayatukuza. Hayo yalitendeka si kwa kificho bali Nyerere akiwa hai  huku akilalalama. Nyerere alilalamika kuwa “…… mazuri tuliyoyafanya wangedumisha na tulipoharibu wangerekebisha…..sasa wanabomoa mazuri na kuendeleza mabaya”(Si nukuu halisi),

Miaka thelathini baada ya Nyerere sasa amekuja Rais Magufuli anayetaka kuirudisha nchi katika reli ya uhuru. Huyo ni Magufuli. Cha ajabu wananchi wengi hawaelewi na wanastuka. Si wa upinzani tu bali hata wa chama chake. Wengi wa wana CCM wanafurahi kuwa rais ametoka CCM na anawakomoa wapinzani lakini sidhani kuwa kwa ujumla wao wanakubaliana na dhana ya kuirudisha nchi katika reli ya uhuru na kuiwekea ‘standard gauge’ ya uhuru. Haionekani dalili ya wana CCM kumwambia Magufuli kuwa sasa ni wakati  wa kupaa na siyo kutembea kwani kwa miaka thelathini tulikuwa nje ya reli. Hakuna dalili ya kuonekana wazi kwa wanaomuunga mkono kwa kusema sasa ni kutumia ‘fast track’ ya kujitegemea na kurudisha ujamaa wetu kwani taifa lisilokuwa na mila wala utamaduni ni mfu.

Magufuli ni Mkristo. Kuna jambo  nimshauri  ambalo lilimpata si Nyerere tu bali sisi watanzania  na nataka kuieleza kwa mfano huu wa Biblia.

 Mungu aliteua kabila lake.Akaliita  Israeli  Akalitetea na kulitukuza. Akawakinga dhidi ya maadui zake. Akawawekea ahadi nyingi zenye matumaini mengi moja ikiwa yeye mwenyewe kuja duniani kama mtu sawa na wao ili kuwa mfalme wao na kuwakomboa kutoka mikono ya mkoloni wao mkuu yaani shetani. Waisraeli waliyasoma maandishi mengi yaliyoandikwa kwa maelekezo ya  Mungu kuhusu ukuu wa Mungu wao, uzuri Wake, ahadi Zake na matumaini yao. Lakini ni Waisraeli haohao aliowateua, kuwatetea na kuwakinga ndiyo waliomsulubisha. Tena wakimsulubisha kwa kusema wanafanya hivyo kwa kumtetea Mungu wao wanayempenda. Ni watu waliokuwa karibu na Mungu ndiyo waliofanya uasi huo. Akina Yuda mhasibu wake mkuu,na  Makuhani walioshika nafasi ya Haruna aliyekuwa na Musa kutoka kabila la Walawi. Musa na Haruna ndiyo waliowatoa Wairaeli hao kutoka utumwani Misri.

Nimenukuu haya kwa sababu moja. Magufuli hakufanya kazi na Nyerere moja kwa moja. Katika kundi la wafuasi wa Nyerere aliowafahamu na kuwapenda na kuwateua na kuwatetea na kuwakinga na kuwasifu kwa kadri ninavyofahamu Magufuli hakuwepo.  Nyerere aliwaachia Reli ya uhuru watu aliowaamini na kuwateua na kuwapamba kama Mungu alivyowafanyia Waisraeli. Kama Waisraeli walivyomfanyia Mungu wao, ndivyo wateule wa Nyerere  walivyomfanyia Nyerere na kuitoa  Tanzania nje ya reli hiyo na Magufuli kuiokota Tanzania ikizagaa kwenye mikono ya wakoloni wa kila namna na kila hila na kutaka kuirudisha tena relini. Tahadhari anayostahili kuichukua Magufuli ni kuwa macho kuona  hasalitiwi na wateule wake kama ilivyotokea kwa Nyerere au Mungu wa Israeli.

 Nyerere kama Mungu wa Israeli alitunga vitabu vingi sana kuhusu sera za ujamaa na kujitegemea na mwelekeo na matumaini ya watanzania. Hakuna Rais Afrika aliyetunga vitabu vya kuwaelimisha wananchi wake kuhusu sera ya nchi yake kama Nyerere.. Kwa hiyo wafuasi waliomsaliti ni wale ambao walisoma vitabu vyake na kuhitimu kwenye vyuo vyake.

Katika wosia wangu huu nitaeleza nini maana halisi ya uhuru na lengo la kudai uhuru. Tanzania siyo Ethiopia au Liberia ambapo huwezi kuwaambia wananchi kuwa tulipata uhuru kwa sababu fulani kwani nchi hizo hazikutawaliwa. Kwa hiyo ukienda Ethiopia utaeleza malengo ya maisha yao bila kutaja mkoloni au uhuru.

Mwaka 1959 na 1960 nikiwa darasa la tatu na nne wakati harakati ya kudai uhuru inapamba moto. Uchaguzi mkuu huru na wa vyama vingi ulikuwa mwishoni mwa 1960 na siku ya uhuru ilikuwa 1961 Desemba tisa . Wakati wa harakati hizo Nyerere na wanaharakati wote wa uhuru walieleza sababu ya kudai uhuru na uchaguzi wa demokrasia. Nilikuwa na umakini zaidi na kuwa na kumbukumbu kwa kuwa kwa takriban miezi sita vikao vya harakati hizo zilifanyika nyumbani kwetu nami nilikuwa na nafasi ya kutafsiri mambo mengine toka Kiswahili hadi Kiiraq na kinyume chake.Mfululizo wa makala haya utajadili kwa nini tulidai uhuru wa Tanzania na wapi tuliteleza na tunateleza jambo  lililofanya Tanzania yenye rasilimali nyingi isiwe kwenye kiwango kimoja cha maendeleo kama nchi za Kenya, na Kore Kusini na hata Vietnam na Ghana.

 Waamerika kila siku wanajikumbusha “THE AMERICAN DREAM” yaani Ndoto ya Marekani ya kupigania uhuru wao  na kuunyakua toka Uingereza kwa nguvu. Kila Rais wa Marekani anapozungumza lazima ataje walau ndoto hiyo ya kupigania uhuru wao na asipofanya hivyo wananchi wa Marekani humkumbusha kwa nini hainukuu ndoto hiyo na haiweki Marekani katika reli ya ndoto yao. Kama taifa kubwa kama hilo iliyonyakua uhuru miaka zaidi ya mia mbili arobaini iliyopita inathamini ndoto zake si zaidi kwa sisi taifa maskini na dogo iliyopata uhuru  chini ya miaka sitini iliyopita kujikumbusha na kuimba ndoto yetu kama sala kila kukicha?

Makala haya yanalenga kuelimisha wajukuu wetu malengo ya kudai uhuru na nini ndoto ya Watanzania wahenga waliodai uhuru. Maraisi wa Marekani hadi Trump wa sasa anadai kuwa anatekeleza mawazo ya “OUR FORE FATHERS”  sisi watanzania tunasahau upesi mawazo ya waasisi wetu kabla hata hawajafa.

Pamoja na malengo haya makala haya yanalenga kumpa pongezi Rais wa sasa kwa kuona hili la kuwarudisha watanzania katika reli ya uhuru wetu. Hata kama hatafanikiwa sana kuturudisha lakini juhudi zake katika nyanja hiyo itatukumbusha kuwa tulishafanya makosa na tunastahili kujirekebisha. Madhaifu ya Rais si hoja yangu hapa kwani hata watakatifu wengi na masahaba wa mitume na manabii sit u walikuwa na makosa bali walikuwa na madhambi makubwa.

Kwa kadri nionavyo na kwa utekelezaji wake Rais Magufuli sasa anaweza kuwazidi akina Kwame Nkurumah wa Ghana mzalendo halisi wa Afrika, Sekou Toure wa Guinea ya Conakry aliyetingisha ukoloni wa ufaransa na hata Nyerere ambao wote walijipambanua kama wazalendo halisi baada ya uhuru wa nchi zao.

Madai hasa ya uhuru hayakutokana na watanzania kuwa hamu ya kumweka mtu mweusi kuwa kiongozi wao ingawa wananchi walitambua kuwa ni fedheha kuwa na kiongozi ambaye hatokani nao. Hata leo ni fedheha kwa mtanzania kutawaliwa na hata mnageria. Hiyo ni hulka tu ya binadamu. Madai ya uhuru pia hayakutokana na madai ya kepepea bendera yetu badala ya ya  nchi nyingine. Madai hayo  mawili yaani ya kiongozi mweusi na bendera yetu yangekuwa ni madai dhaifu na kama vile ngoma ya watoto haikeshi hayangetufikisha kwenye uhuru kwa kuwa hayazingatii mahitaji na maendeleo ya binadamu bali ni urembo tu yaani’ cosmetic.’

Madai ya uhuru ambayo wahenga walizungumzia wakati wa harakati za uhuru ni mahitaji ya maendeleo ya wananchi wote kwa nchi nzima kwa kujiongoza wenyewe kwa uhuru na kuchapa kazi kwa bidii na kupata mapato ya haki kutokana na jasho letu.

Wakati wa madai ya uhuru kabla hatujapata uhuru ndipo maneno “UHURU NA KAZI” yalipozaliwa ingawa kitabu chake kilitungwa tu mara baada ya  uhuru na ni kitabu cha kwanza cha Nyerere kuhusu sera ya TANU. Maana yake maneno hayo ni UHURU NI KAZI. Nyerere hakuwa mlaghai. Kwa hapo namfananisha na Magufuli. Hakuwadanganya watanzania kuwa baada ya uhuru kuna vya kugawana tu bali aliwaambia watanzania wote kwa uwazi kuwa uhuru wetu utakamilika tu kwa kuchapa kazi kwa kushirikiana na kwa umoja wetu. Nyerere alizungumzia uzalishaji wa bidhaa na huduma, alizungumzia uthibiti wa rasilimali za nchi na kuzitumia kwa faida ya wote, alizungumzia taifa litakalojitegemea na siyo ombaomba. Nakumbuka alipofika Bashnet 1960 katika kiwanja ambacho leo imejengwa nyumba ya wageni ya Masabeda Guest House  ambapo alimnadi mgombea wa ubunge Amri Dodo wa TANU dhidi ya Herman Sarwatt wa kujitegemea Nyerere alitumia muda mrefu siyo kumnadi Dodo  bali kueleza malengo ya kudai uhuru na matumaini ya watanzania. Aliainisha bayana kuwa malengo yetu ni kuchapa kazi na kujitegemea kwani tuna rasilimali nyingi zilizosababisha wakoloni kututawala na hizo pia ni sababu ya sisi kumwondoa.. Hapo ni kabla ya uhuru na Nyerere alikuwa wazi kwenye hilo.

Lakini kuchapa kazi na kutumia rasilimali zetu ambazo kwayo wakoloni walikuwa wanafaidika nazo haingekuwa rahisi kwa Nyerere, Nkurumah, Sekou Toure na akina Patrick Lumumba wa DRC. Baada ya uhuru hapo ndipo vita vilipoanza kati ya Marais hao na wakoloni. Lakini wakoloni hawakuwa peke yao bali walikuwa na wenzetu ambao walikuwa pia wateule wa Nyerere, Nkurumah, Lumumba na Toure. Na ni hawa ambao baada ya viongozi hao kutokuwa madarakani  waliitoa nchi zao kutoka reli ya uhuru na sehemu yake ni hao ambao Magufuli amewakuta madarakani na ambao ni sehemu ya wateule wake anaowatumia anapotamani kuirudisha Tanzania kwenye reli hiyo na kuiboresha. Mifano iliyohai ni wateule wa Lumumba  kina Jenerali Mobutu, na wateule wa Nkurumah kina Jenerali Achiempong na wengine.

INAENDELEA WIKI IJAYO

    END…………….MWISHO

Jacob Qorro ni mwalimu na mchumi. Ni mchambuzi wa Uchumi Siasa wa Maendeleo  (Political economy of Development) na mambo ya jamii. Anapatikana simu namba 0786 151385

(SEHEMU YA PILI)

(Wiki iliyopita katika makala hii sehemu ya kwanza  tulizungumzia sababu ya waafrika hususan Tanzania kudai uhuru. Leo tutazungumzia sababu kuu ya kutawaliwa kwetu ili baadaye tuone mgongano unapotokea kati ya maslahi yetu ya kufikia ndoto yetu ya uhuru na maslahi ya mabeberuna baadhi ya  viongozi wetu na kuona wananchi wanajigawaje kati makundi hayo.)

Kauli ya mwingereza  aliyekuwa bepari na mmiliki wa baadhi ya mashamba makubwa, migodi ya madini na makampuni ya biashara Kusini mwa Afrika, Cecil Rhodes, ambapo kwa heshima yake waingereza waliita Zambia Northern Rhodesia na Zimbabwe Southern Rhodesia itatupa sababu kuu pekee ya kwa nini Tanzania  na Afrika ilitawaliwa. Rhodes, mwana wa familia maskini  akiwa na elimu kidogo ya miamba alitembelea nchi hizo za Kusini mwa Afrika  wakati ambapo madini Afrika Kusini yalikuwa yanapatikana ovyo mitoni kama ilivyokuwa Tanzania ambapo wananchi walikuwa wanachezea bao kama kete.

Mwingereza huyo aliona rasilimali nyingi za madini,ardhi nzuri kwa mazao ya kilimo na hali ya hewa safi kuzalisha malighafi zilizokuwa zinahitajika uingereza iliyokuwa inakua kwa kasi kiviwanda. Alijiridhisha kuwa matatizo mengi ya uingereza yataisha iwapo uingereza itapata rasilimali hizo. Uingereza ilikuwa na matatizo ya kupata malighafi za viwandani na ukosefu wa ajira. Aliporudi Uingereza aliitisha kikao Mashariki mwa Mji  Mkuu wa London wanapoishi maskini wengi akiwemo yeye.

 Uingereza ni kisiwa ambapo upepo wa westerlies unavuma toka Kusini Magharibi kuelekea Kaskazini Mashariki karibu kila siku. Na kwa viwanda vibovu vya wakati ule ambapo moshi wa viwanda vinavyotumia  makaa ya mawe kama nishati ulitanda  sana na kuchafua hewa. Matajiri walikuwa wanaishi upande wa Magharibi mwa London kusiko na moshi wa viwandani na maskini akina Cecil Rhodes upande wa Mashariki panapoelekea moshi wa viwandani. Hayati Brigedia Adam Mwakanjuki aliyekuwa Kamanda wangu kambi ya Makutopora aliiita London Mashariki Manzese ya London wakati Manzese ya Dar es Salaam ilipokithiri kwa uchafu.

Baada ya kusikia kilio cha maskini hao wa London cha ukosefu wa ajira na njaa kali kiasi kuwa hawana mkate chakula chao kikuu,Cecil Rhodes alieleza   aliyoyaona Afrika na kuhitimisha kuwa ili kuondoa matatizo ya Uingereza ya umaskini na ukosefu wa mali ghafi na kwa kuwa  kisayansi huwezi kuhamisha rasilimali hizo toka Afrika kwenda ulaya wala kubadilisha hali ya hewa hiyo kwenda uingereza na ili Uingereza iwe nchi yenye nguvu kiuchumi na kijeshi kwa Uingereza kuwa na koloni katika sehemu hiyo ya Afrika ni swala la mkate na siagi (for Britain to have a colony in that part of Afrika is a bread and a butter question). Akaongezea kuwa ili kufanikisha lengo hilo lazima ramani ya Afrika toka Cairo hadi Cape Town ipakwe wekundu (the map between Cairo to the Cape should be painted Red). Wekundu maana yake ni bendera ya Mwingereza iitwayo Union Jack. Kwa maana ya Cecil Rhodes kupaka ni kupeperusha bendera ya mwingereza katika maeneo yote kati ya Cairo ya Misri hadi Cape Town ya Afrika Kusini yaani kutawala Misri, Kenya, Uganda, Tanzania, Zambia, Malawi, Zimbabwe, Botswana, Lesotho Swaziland na Afrika ya Kusini. Na kutawala nchi hizo ni jambo la mkate na siagi kwa mwingereza au jambo la ulwa au kufa na kupona.

Rais yeyote anayetawala Afrika akiwemo Magufuli aelewe kuwa hadi leo kwa mkoloni  kupata malighafi zetu ni jambo la kufa na kupona kwa kuwa bado wanahitaji malighafi na kuwapatia ajira wananchi wao.

Magufuli na wenzake pia waelewe kwetu sisi waafrika tukiwemo watanzania kutumia rasilimali zetu ili kufikia malengo na ndoto zetu “ The African  Dream”  au “TANZANIAN DREAM”  ni jambo la kufa na kupona kwani sisi pia tunahitaji mkate na siagi.

Kwa hiyo ni juu ya Rais aliye madarakani na watanzania kuamua kuchagua kupeleka mkate na siagi kwa nani, nyumbani kwetu na watoto wetu au kwa wakoloni na watoto wao. Rais akitupa mkate na siagi ndiyo uhuru wetu unakamilika na akiwapa wakoloni ndiyo uhuru wetu unapungua na ukoloni unatamalaki.Kwa hiyo siasa ya  ili hali mtu mweusi tu yuko madarakani na bendera inapepea yaani ‘cosmetic freedom’,yaani  uhuru wa urembo au uhuru bandia siyo lengo la kudai uhuru. Pia tusidanganyike kuwa tuna mabeberu wastaarabu.  Natoa mifano.

Leo wachina wanahitaji sana malighafi toka Afrika kuliko hata Marekani na Uingereza. Na njia pekee ya kupata rasilimali hizo ni kuelewana na viongozi wa kiafrika vizuri na ikiwezekana kuwapamba. Ili kupata rasilimali hizo kwa uhakika na katika dunia ya leo China haiwezi kuifanya Afrika kuwa koloni lake rasmi bali ni kutumia ujanja wa kuwaweka sawa waafrika ili waipe nchi hiyo malighafi inayotaka. Kwa hiyo China itatoa masharti nafuu ya biashara hiyo mojawapo ni kutojali kuuliza jinsi tunavyojiongoza hata kama tutauana kwa mamia. Kwa hiyo viongozi wengi wabovu wa Afrika wanaona kuwa China ni nchi poa kwa kuwa haiulizi haki za binadamu walauongozi bora wala demokrasia. Hata Marekani. Trump anapoona makosa yamefanywa na swahiba wake Saudi Arabia atazungumzia maslahi ya Marekani ni muhimu kuliko watu kadhaa waliouawa kikatili na Falme hiyo lakini kosa dogo la Iran ataihangaisha dunia hadi Umoja wa Mataifa na sisi tutamwitikia.

Leo Japan ina mashindano na msuguano wa kibiashara na nchi za Ulaya na Marekani kwani nao wanazalisha bidhaa ambazo Japan inataka kuwauzia. Kontinenti pekee ambapo Japan inaweza kuuzia magari yake na vifaa vya electroniki bila msuguano ni Afrika kwa kuwa  waafrika wengi hawajafikia kiwango cha kuzalisha bidhaa zinazofanana na za Japan. Kwa hiyo Japan lazima itafute koloni la soko lake  na Afrika ni mwafaka kama koloni hilo ili kuhakikisha hakuna gari nyingine isipokuwa ya kijapani katika barabarani za makoloni yake hayo.  Kwa hiyo Japan haitapenda kusuguana na viongozi wa Afrika na wakitaka misaada wanatazama mizania ya biashara kati yetu.Baada ya kuona wana faida kubwa na  ili ukoloni huo uendelee huchukua sehemu ndogo tu kutujengea madaraja matano nasi tunaona dili kweli.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                   

Kwa nini wakoloni walileta watu wao kututawala? Jibu ni kuwa kuleta watu wa kututawala kutoka ulaya ni ghali na wakoloni wasingependa kuwaleta. Sababu pekee ni kuwa uwepo wa watu wao unawahakikishia utiifu wetu kwa nchi tawala kwani kuna mashindano ya makoloni toka miaka ya 1800 hadi leo. Ili kuhakikisha sisi tunabaki chini ya mwingereza waingereza walileta magavana na wengine.Lakini pia walitumia machifu wetu waaminifu kwao kututawala ili kupunguza gharama zao na kutuhadaa kwamba tunashirikiana kwenye utawala.

Pia wakoloni walijenga miundombinu kama shule na zahanati ili tupate huduma na tuwatumikie zaidi.

Kuna aina tatu za ukoloni. Kuna ukoloni wa kutawaliwa na kuwekewa viongozi kwenye kila ngazi na kupeperusha bendera. Huo ukoloni kwa mwingereza haukuwa muhimu sana hadi anapoona kuna hatari ya mirija yao ya unyonyaji kuzibwa au kukatwa.

Kuna ukoloni wa akili au kasumba.Huu ndiyo ukoloni mkuu ambao Magufuli atashindana nao kwa miaka yote atakapokuwa madarakani kwani nao ni endelevu na hubadilikabadilika yaani ni ‘dynamic’. Ukoloni huo uko ndani na nje ya CCM. Maneno “haiwezekani”, “hatuwezi” “ni haki yao siyo yetu” ni kauli ya wasomi wengi Kwa mfano, msomi mwanasheria Mtanzania anapotetea unyonyaji wa makampuni ya madini kuliko hata wenye makampuni hayo ambao siyo watanzania  na hata pale wenye  makampuni wanapokuwa tayari  kujadiliana na serikali wasomi hao bado wanaona wenye makampuni hayo wanakosea ujue kuwa hatuna wasomi bali wenye kasumba.

Ukoloni huo  utampa wakati mgumu  Magufuli kwa kuwa umejikita zaidi si vijijini bali kwa wasomi ambao lazima awateue kuendesha serikali yake. Hatari ni kuwa wasomi hao watakuwa wanafanya kazi kwa mashaka na wasiwasi na  siyo kwa mbwembwe kama bosi wao anayejiamini. Sioni ajabu kwa nini Magufuli hamwachii Paul Makonda hata pale anapoonyesha mapungufu ya dhahiri. Ujasiri na uthubutu wa kutenda jambo jema bila kubabaika ili hali anamini kuwa ni la maendeleo ndiyo kinachompendeza mtanzania wa leo akiwemo Magufuli. Nadhani hata uagizaji wa makontena yale ilikuwa sehemu ya jitihada zake isipokuwa hakuzingatia utaratibu.

Ukoloni mwingine ambao ndiyo chanzo na mama wa ukoloni wote ni ukoloni wa uchumi. Tulitawaliwa ili tunyonywe rasilimali na jasho letu. Tunyonywe ardhi, madini, mito na vivutio vyetu.  Unyonyaji huo wa uchumi uko aina mbili. Ukoloni wakati tunatawaliwa yaani ubeberu na unyonyaji wakati tuna kiongozi mwafrika mweusi na bendera yetu  na huu ni ukoloni mamboleo.

 Wakati tunatawaliwa wazungu na machifu wetu ndiyo walisimamia unyonyaji huo. Baada ya uhuru unyonyaji huo ndiyo inasimamiwa na viongozi tuliowachagua wenyewe (wanisamehe). Kama mkoloni alituambia tulime pamba kwa wingi na akatusimamia na akafaidika na leo anayetuambia tulime pamba kwa wingi na kutusimamia ni nani?Nisieleweke vibaya. Kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha malighafi kwa wingi siyo ukoloni kwani hata wao wanafanya hivyo.

 Ukoloni ni pale tunapokuwa huru na kukosa malengo ya malighafi zetu bali tunakubaliana na matakwa ya mkoloni. Akina Mirambo na Mkwawa na wengine walikuwa na rasilimali na walijua namna ya kuzitumia. Wabena waliuza majembe siyo chuma. Wenye nyuzi na magamba ya miti waliuza nguo kwa wenzao siyo magome ya miti wala nyuzi. Kwa hiyo jamii zetu kabla ya wakoloni zilikuwa na viwanda.Kule India Mahatma Gandhi waziri Mkuu wa kwanza aliwaambia watengeneze nguo zao za asili na waachane na nguo za ulaya ili kufufua viwanda vyao vilivyouawa na wakoloni. Tena alifanya hivyo wakati anadai uhuru siyo baada. Alikuwa mwazi kuwa uhuru ni wa uchumi na siyo rangi ya mtu wala bendera. Lakini sisi miaka sitini baada ya uhuru hatuna uhakika tufanye nini na uhuru wetu.

Wakati wa ukoloni wakoloni walohakikisha kuwa uchumi wetu umegundishwa kwenye uchumi wao na akili za wasomi na viongozi wetu pia imezubaishwa kwenye matakwa yao na kuwa ingawa tutakuwa huru  siyo rahisi viongozi wetu kubandua uchumi wa Afrika na Tanzania kutoka ubao wenye gundi kali yaani uchumi wa wakoloni na siyo rahisi kuondoa kasumba zao kutoka matakwa yao kwa hiyo maraisi wengi wa Afrika na huenda pia Tanzania walifanya kazi ileile waliyokuwa wanafanya machifu wakati wa ukoloni tofauti tu ikiwa viongozi wa sasa wamesoma na wanapeperusha bendera murwa kwenye magari yao.

Maraisi wengi wa Afrika ni makuwadi wa kugawa mali zetu ili mradi wasifiwe na mataifa ya nje. Kwenye matatizo ya marais wa Afrika Magufuli kwa uhakika amejipambanua kuwa hayuko.

INAENDELEA WIKI IJAYO

Jacob Qorro ni mwalimu na mchumi. Ni mchambuzi wa Uchumi Siasa wa Maendeleo(Political Economy of Development) Anapatikana kwa simu 0786  151385

END………….MWISHO

(SEHEMU YA TATU)

Wiki iliyopita tuliona kwa nini tulitawaliwa na jinsi ilivyo ngumu kubandua uchumi wa Afrika kutoka uchumi wa Wakoloni lakini kuwa Rais Magufuli anajitahid ikufanya hivyo.Leo tuone jitihada walizofanya akina Nkurumah, Sekou Toure, Lumumba na Nyerere katika kuitoa Afrika katika gundi hiyo na matatizo waliyoyapata

Kwame Nkurumah wa Ghana rais mweusi wa kwanza aliyeipatia nchi yake uhuru nayo ikiwa nchi ya Afrika ya Kwanza kupata uhuru ni rais msomi aliyekuwa na muono wa hali ya juu kuhusu nchi yake na Afrika kwa ujumla.

Ghana haikuwa nchi ya kwanza Afrika kupata uhuru lakini nchi nyingine zilizotangulia Afrika zilikuwa za Afrika Kaskazini ambazo ni nchi za kiarabu kama vile Misri, Morocco Libya na Tunisia.

  Baada ya Uhuru wa Ghana 1957, Nkurumah alianza mwenyewe harakati ya kupigania uhuru wa nchi nyingine za Afrika akisema wazi kuwa uhuru wa nchi ya Ghana hauna maana na haujakamilika bila Afrika yote kuwa huru, msemo ambao Nyerere aliutumia sana hasa baada ya Nkurumah kupinduliwa na Mteule wake mpenzi Jenerali Achiempong’.

Rais huyo wa Ghana alitunga vitabu vya kiuchumi vingi sana. Tunaweza kuviita vitabu vya ukombozi wa Afrika kwa sababu, kwa mfano, katika kitabu chake kimoja ambacho kiliwastua wakoloni kuwa sasa waliona watakosa malighafi za Afrika wakimwachia Nkurumah aendelee  kuwaelimisha marais wenzake wa Afrika kuwa kila swala la uhuru ni swala la uchumi, kiitwacho Neo Colonialism, The Last Stage of Imperialism  yaani Ukoloni Mamboleo Ngazi ya Mwisho ya Ubeberu Kwame Nkurumah aliwakumbusha viongozi wa Afrika kuwa wanapopata uhuru watawale na kukomboa  uchumi kama Mahatma Gandhi wa India.

Wakoloni hawakumchelewesha hasa pale alipoamua kumsaidia mwamba mwenzake Sekou Toure wa Guinea aliyeadhibiwa na Wafaransa kwa kung’oa kila kitu maofisini na kuharibu miundombinu za kuongoza nchi kwa kuwa alikataa kuwa ndani ya himaya ya nchi zinazozungumza lugha ya kifaransa baada ya kupata uhuru.Nkurumah alipinduliwa kwa kumtumia swahiba wake na mteule wake Jenerali aliyemwamini sana Achiempong’.

Baada ya mapinduzi hayo wakoloni wakawaelekea waafrika na kuwaambia kuwa hawaoni kuwa hata waafrika hawapendi mawazo ya kijinga ya Nkurumah? Hapa tujilaumu.

Wafrika ni watu wa shamrashamra. Kwa mfano Jenerali Ironsi aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Nigeria baada ya kutoka Tanzania kuja kuunda Jeshi la Wananchi wa Tanzania baada ya maasi ya 1964 alipindua serikali ya nchi yake na watu wa Nigeria wakamshangilia. Baada ya muda Mfupi akapinduliwa na Jenerali Yakub Gowon na watu wakamshangilia Gowon. Mwandishi moja wa Gazeti la The Transition Peter Enahoro akaandika kuwa sisi waafrika ni wa ajabu kwani ni watu walewale waliomshangilia Ironsi ndiyo waliomshangilia Gowon na kuhitimisha kuwa katika Afrika kushangilia hakuonyeshi kupenda au kuchukia bali ni hulka tu za shamrashamra.

Mapinduzi hayo ya Nkurumah yaliwakatisha tama sana waghana na waafrika kwa ujumla  kwani yalifuatiwa kwa karibu sana na mapinduzi ya nchi ya kwanza huru kupinduliwa , Togo ambapo Ufaransa walikuwa na mkono sana baada ya kuona kuwa Rais aliyechaguliwa anataka kumwiga Toure wa Guinea. Kwa hiyo marais wote wa Afrika waliofuata wakawa na woga wa kutekeleza yale yaliyokusudiwa na madai ya uhuru. Cheo na madaraka na mshahara na hadhi ya Rais ni tamu. Nani asiyetaka kuwa na hivyo? Pamoja na marupurupu makubwa hata wanajeshi wanatamani nafasi hiyo ya juu ya urais. Na ndivyo ilivyokuwa Afrika. Jinsi marais walivyotegemea wanajeshi kulinda uhuru ndivyo wanajeshi walivyoingiza kichwa, mabega kiwiliwili na baadaye mwili mzima kwenye utamu wa siasa. Chukuli India ambayo viongozi wake hawajawahi kutumia jeshi katika siasa na Pakistan ambapo walitumia sana wanajeshi na sasa jeshi likiona ubishi wa siasa unazidi wanamwarifu waziri mkuu kuwa wamalize ubishi au watachukua hatamu za uongozi. Hii ni kweli hata Sudan Kaskazini.

Marais waliokuwa madarakani wanataka kubaki madarakani hata kama hawatekelezi ndoto za uhuru.Wananchi wanataka ndoto zitekelezwe. Utekelezaji unataka kujitolea mhanga kwa wananchi hasa watumishi wa serikali  kuwa tayari kuacha marupurupu waliyozoea wakati wa ukoloni lakini watumishi hao wanamwona rais huyu kashindwa kazi na wanataka waendelee na mfumo wa kikoloni kwa kuwa unawafaidi wao ili hali wananchi wanataka kuona matunda ya uhuru na rasilimali zao. Wakati hayo yakiendelea taasisi ambayo tayari ina uzoefu wa kujiongoza yenyewe kwa muda mrefu na ina bunduki yaani taasisi ya Jeshi nalo linaona kuwa linaweza kupata nafasi ya kujipenyeza kwenye siasa kwani wakati rais huyo anatishiwa na wananchi hutegemea majeshi ya nchi yake. Kwa hiyo baada ya mapinduzi ya Ghana nchi za Afrika Magharibi,pamoja na usomi  mkubwa wa wananchi wake zote zilipinduliwa. Hiyo iliwafanya viongozi raia wanayeingia madarakani kuachana na ndoto ya uhuru wa Afrika na kuwatumikia wakoloni. Hii ilileta chereko kwa wakoloni na kwa takwimu za kupikwa walizitangaza nchi hizo kuwa na sera nzuri na uchumi unaokua sana.

Wakati Nkurumah alipopinduliwa wakoloni walinyosha kidole kuwa waafrika wanashangilia kuondoka kwa dikteta na mnyanyasaji wa wananchi wake.

Nkurumah alifanyia nini Afrika ?Katika vitabu vyake alionyesha, tena kwa takwimu za uhakika, jinsi uchumi wetu unavyonyonywa kwa uchimbaji wa madini na uuzaji wake akionyesha dhahiri kuwa kuna mahusiano ya kibiashara kati ya wachimbaji na wanunuzi na mabenki ya biashara yenye kutoa mitaji ambapo madini ya dunia nzima yako chini ya mfumo na utawala moja.Alielezea pia kuwa mali ghafi za Afrika lazima zichakatwe ili siyo kutengeneza tu  bidhaa iliyochakatwa na  ziuzwe nje bali bidhaa halisi za mlaji. Kwa mfano alitaka Ghana kutumia Kakao yake si kutengeneza unga wake wa kuuzia nje bali kutengeneza chokoleti na madawa yanayotumia kakao. Kwa hiyo aliishauri Afrika kuwa na viwanda badala ya kutumikia viwanda vya wakoloni.

Ili kufanikisha jambo hilo Nkurumah alisisitiza sana Afrika kuungana haraka ili kuwa na soko kubwa kwa bidhaa zitakazozalishwa Afrika. Kilichomponza zaidi ni pale alipozuia kokoa ya Ghana iuzwe ulaya kwa bei wanayotaka wao  na kutaka ichakatwe Ghana lakini wazungu walishusha bei ya kokoa ghafi na iliyochakatwa na wananchi wakalalamika kukosa fedha kama walivyozoea. Wananchi wengi hawaelewi kuwa ingawa malengo ya uhuru ni matamu uchungu ni moja ya njia za kuyafikia, na uvumilivu unatakiwa.

Wakati Ghana inapata uhuru wake Guinea ya Conakry iikuwa inajiandaa kufikia hatua hiyo na 1960 ikajitawala. Rais wao wa kwanza Ahmed Sekou Toure alikataa kuendelea kuwa mtiifu kwa Wafaransa. Alieleza kwa watu wake kuwa ni heri kukaa katika umaskini kuliko fedheha ya uhuru bandia na watu wa Guinea walikuwa waaminifu sana kwake na kwa miaka mingi aliendesha nchi kwa tabu sana huku akiwa na vikwazo vingi. Nkurumah wa Ghana alimsaidia kifedha na wakoloni walitumia mwanya huo kuwa anachezea fedha za Ghana.

Patrick Lumumba wa Congo pia alipata sulubu hiyo na kuuawa na wakoloni tena kwa kuwatumia marafiki zake wa karibu kw sababu ya kutaka kuthibiti utajiri wa madini wa nchi yake ili iwanufaishe wananchi wake.

Mwalimu Nyerere akiyaona hayo ya marafiki zake alianza kuwaelimisha watanzania kila jambo linalotakiwa na kuanza kutumia fedha nyingi ili kuwapeleka viongozi wa ngazi zote na katika kada na fani na taasisi zote za umma katika semina ili waelewe mwelekeo wa siasa inayotakiwa na kuwakumbusha sababu ya kudai uhuru au  Tanzanian Dream. Nadhani matumizi ya fedha kwa ajili ya semina, warsha na makongamano yalishamiri sana wakati wa Nyerere. Haya siyo mapungufu. Ilibidi kila mtu aelewe nafasi yake katika taifa. Wanajeshi wajue wanastahili kufanya nini kama walinzi wa taifa. Watumishi wajue wanatumikia sera ipi na kwa malengo gani, Licha ya semina mwalimu na chama cha TANU walitoa maandishi mengi sana. Kwa hiyo hata mwanafunzi darasani alikuwa anajua nchi inakoelekea.

Kuna maswali Nyerere alijiuliza na kuyajibu kwa vitendo . Kila mtu anajua kuwa kabla ya uhuru jamii zetu hazikuwa ombaomba. Kila mtu anajua kuwa wakati wa ukoloni sehemu kubwa ya mali tuliyoizalisha iliende kuendeleza Uingereza kuliko Tanzania. Tuseme kuwa mali hiyo ni 60%. Kila mtu anajua kuwa sehemu ndogo tu ya mali hiyo ilitumika Tanzania kuendesha utawala na huduma kama afya na shule na ujenzi wa barabara. Tuseme hiyo mali ni 40%. Kila mtu anajua kuwa wakati wa ukoloni Tanzania haikuwa ombaomba pia. Labda tulikuwa wakopeshwaji. Baada ya uhuru  Tanzania inastahili kutumia mali zote yaani 60%+40%= 100%. Hii habari ya sisi kuwa ombaomba imetoka wapi wakati tuko huru?

Nyerere aliwakimbiza sana watanzania katika kuhakikisha kuwa uhuru ni kazi. Waingereza walioalikwa mwaka 1971, miaka kumi baada ya uhuru, viongozi waliokuwa magavana, Ma  PC (wakuu wa Mikoa) na Ma DC walikubali kuwa kazi imefanyika. Wakati huo Nyerere alikuwa na wasomi wachache sana katika uongozi wake. Nakumbuka DC wangu Mbulu na Babati , Laizer, alikuwa dereva wa mabasi kabla ya uhuru. Sote tunaelewa kuwa akina Kawawa hawakuwa na Elimu ya kutisha lakini walikuwa na utumishi wa kizalendo uliotukuka. Rasilimali zilizoenda Uingereza Nyerere alianza kutumia kuendeleza Tanzania.Wakati huo rasilimali nyingi zilikuwa bado hazijachimbwa au kulimwa kwa ufanisi kama sasa. Lakini nchi ilielekea vizuri.

Baada ya 1971 viongozi wateule wa Nyerere walianza kufanya kazi kwa mazoea na kuingia tamaa Uchumi ulianza kuharibika kabla ya Nyerere kutoka madarakani. Ilikuwaje? Kahaba Siasa ndiyo iliyoifanya Tanzania ikose mwelekeo wake toka enzi ya Ujamaa na Kujitegemea na Ufisadi ukamaliza nchi kabisa hata juhudi za Hayati Sokoine hazikuzaa matunda. Sokoine aliikuta Tanzania kama Mikael Gorbachyiev wa alivyoikuta Urusi iliyosambaratika alivyokuta nchi yake aliposhika uongozi.

WIKI IJAYO TUTAONA JINSI SIASA KAHABA NA UFISADI KWA PAMOJA VILIVYOTUANGUSHA.

END………………………..MWISHO

Author: admin