YA WAPI?

YAWAPI leo yawapi, ninaomba kuambiwa
Nikwache hani kwa lipi, nachelea kuuguwa
Mwengine katu simpi, apendwae huambiwa
Yaliyoyakienziwa, zama hizi yakowapi?

YAWAPI yale mapenzi, mapenzi yasiovisa
Apendwae kuyaenzi, akazidisha hamasa
Mtu siingwe ja nnzi, eti kisa hana pesa
Sebu mapenzi ya sasa, bora ya enzi na enzi

YAWAPI yasioinda, niyafuate yalipo
Hiyapata nitaganda, simwachi mtu endapo
Hadi wanivishe sanda, taweka kwake kiapo
Aendapo nami nipo, simwachii hata nyanda

YAWAPI leo mapenzi, ya wawili kupendana
Mtu kungiwa simanzi, mpenziwe akinuna
Na kujitia kitanzi, pindi wakifarakana
Zama hizi sijaona, umejaa upuuzi

YAWAPI ninauliza, yale mapenzi asili
Ya kucheka na kucheza, wakutanapo wawili
Yakijiri ya kukwaza, mkwaza katu halali
Hata kama kwa dalili, msiache kunijuza

YAWAPI leo mahaba, yaliojaa huruma
Nyoyoni yaliokaba, yakakamata mitima
Hawanayo kina baba, pamoja na kinamama
Mapenzi sasa nakama, kupenda mtu msiba

YAWAPI hebu nambani, yale yalopoza nyoyo
Kuyapata natamani, nimpate alonayo
Mapenzi ya kizamani, si haya ya mambo leyo
Alau nikonge moyo, nifurahike jamani

YAWAPI natamatia, kalamu naweka chini
Moyo wangu waumia, paumapo sipaoni
Kila nikiangalia, fulani kama fulani
Sijebaki laitani, inamazonge dunia

FATIMA M. MOHAMMED
(Msibahati)
☎️+96879934356
+2551717429891

Author: Gadi Solomon