Yasingekukuta


Yote unayo hutubu, niwapo nina yapata,
Nawe nikajitanibu, muda nakiutafuta,
Matusi kubwa sababu, na fitina unolota,
Wala yasinge kukuta, ungakuwa na adabu.

Kuna kinacho kusibu, ukawa kiburi hata,
Umayatupa mashibu, ja mtupa kotakota,
Kwetu twaona ajabu, nini kimekukamata?
Wala yasinge kukuta, ungakuwa na adabu.

Usambe siye mabubu, kwa huku kujikunyata,
Tunayo mengi mujibu, ukizidi utajuta,
Haja yangu kukutibu, ndwezi iliyo kupata,
Wala yasinge kukuta, ungekuwa na adabu.

Komea hapo muhibu, kama hutaki matata,
Sichezewi na kalubu, hasira zinikituta,
Viwavyo tamuadhibu, kama napiga ufuta,
Wala yasinge kukuta, ungakuwa na adabu,

Vita kwangu uraibu, sio hivi vya kauta
Kamwe havinipi tabu, ugani vinapo kita,
Engeto kuwa kidhabu, utajakuwa mkata,
Wala yasinge kukuta, ungakuwa na adabu.

Dunia nyumba ya tabu, makele haya kamata,
Wengi imesha adhibu, mawi walio tafuta,
Kinwa kina kughilibu, mbasizo watakuwata,
Wala yasinge kukuta, ungekuwa na adabu.

Tamati ndimi tabibu, nizifumbuae tata,
Taadhima ni wajibu, ukitoa utapata,
Ukija umesharabu, utaligumia tuta,
Wala yasinge kukuta, ungakuwa na adabu.

          MKANYAJI
       HAMIS AS. KISAMVU
      kissamvujr@gmail.com
    0715311490/0784311590
   

Author: Gadi Solomon