Yuno Mwambi


Nili nikele pekele, hamuwaza yuno mwambi,
Vile ana makelele, na wingi wa jambijambi,
Hana nyuma wala mbele, kumbe yu ngali sombombi,
Ana kembe yuno mwambi, thama hashiwi kelele.

Mwambaji hasa awile, zimetimu tumbitumbi,
Hulitumbuza nenole, lisiwe kama uchambi,
Wengine liwachokole, kwa maneno ya uchimbi
Ana kembe yuno mwambi, thama hashiwi kelele.

Makaliye nipekule, yana upambaupambi,
Latuhadaa umbole, wala si mrume ngambi,
Mvuli huwaje vile, na maharimu magombi.
Ana kembe yuno mwambi, thama hashiwi kelele.

Na yeo niwafunule, yuno mwana chakubimbi,
Ndiye asongile ndwele, wakasambaa ja simbi,
Akawatusi wavyele, akamba huno ulumbi,
Anakembe yuno mwambi, thama hashiwi kelele.

Kwa yano niyaonile, hafananile na jimbi,
Msongo ummemile, ana haha kila kumbi,
Uchao ni yaleyele, kama mpiga ugimbi,
Anakembe yuno mwambi, thama hashiwi kelele,

Hapano ni tamatile, si mnena tarahambi,
Simi msozwa kusile, ja taa na kumbikumbi,
Na yuno tena simbile, yu pumbe mithili mumbi,
Anakembe yuno mwambi, thama hashiwi kelele.

                 

Author: Gadi Solomon