Zijue fursa ndani ya Mpango Mkakati wa Taifa wa kubidhaisha Kiswahili

Nabil Mahamudu na Loveness John

Serikali ya Tanzania kupitia wizara zenye dhamana ya utamaduni, imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili katika kutekeleza mambo mbalimbali ya ukuzaji na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Miongoni mwa mambo yaliyobainishwa ni pamoja na kuwasajili wataalamu wa Kiswahili katika kanzidata na kuwatumia kikamilifu, kutoa mafunzo ya kunoa stadi kwa wataalamu wa nyanja mbalimbali katika Kiswahili (mfano, wakalimani wa lugha ya kawaida na lugha ya alama, wafasiri, walimu wa kufundisha Kiswahili kwa wageni, wahariri).

Pia kuandaa vitendeakazi vya kuwezesha ubidhaishaji wa Kiswahili kwa maana ya kuandika vitabu vya kufundishia na kujifunzia wageni, kuwezesha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kusaidia maendeleo ya Kiswahili.

Vilevile kuandaa miongozo ya kufundishia na kutafuta fursa mbalimbali zinazohusiana na Kiswahili kwa wataalamu wa Kiswahili ikiwa ni pamoja na kuwazamisha wakalimani katika jamiilugha.

Mkakati huo unalenga kuwawezesha na kuwajengea uwezo wataalamu na wamilisi wa lugha ya Kiswahili pamoja na wadau mbalimbali walioko ndani na nje ya nchi kunufaika na fursa zilizopo kwa manufaa yao wenyewe pamoja na taifa kwa ujumla. Aidha, mkakati utachangia katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utamaduni ambayo itaweka vivutio kwa watu binafsi na mashirika mbalimbali kuchapisha na kusambaza maandiko katika lugha ya Kiswahili na kutafiti.

Aidha kuendeleza matumizi ya lugha hii kwa kuipatia nyenzo na fursa za kuimarisha matumizi yake. Mkakati huu umelenga kuleta mageuzi katika sekta ya utamaduni ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na Kiswahili kama vile machapisho mbalimbali, wataalamu na wamilisi wa Kiswahili kwa lengo la kuifanya lugha ya Kiswahili na mazao yake kuwa bidhaa za kibiashara na hivyo, kuongeza pato la Watanzania.

Utekelezaji wa mkakati huu umelenga kufikia malengo ya kimataifa ifikapo mwaka 2031. Maandalizi ya Mkakati huu yameshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu wa serikali kwa maana ya wizara husika, wahadhiri kutoka vyuo vikuu, jukwaa la wadau pamoja na vyama mbalimbali vya Kiswahili vilivyomo nchini.

Ni matumaini yetu kuwa, utekelezaji wa mkakati huu utakuwa na tija kwa Watanzania, asasi, wadau mbalimbali pamoja na kuongeza pato la Taifa

Ikiwamo ufundishaji Kiswahili kwa wageni.

Miongoni mwa fursa zinazozalishwa kupitia mpango mkakati wa kubidhainisha Kiswahili ni kupata wataalamu wa Kiswahili ambao watahusika kutoa mafunzo kwa wageni ambao Kiswahili ni lugha yao ya pili kujifunza.

Wataalamu hawa watazalishwa kupitia kanzidata ya wataalamu inayosajiliwa na Bakita.

Halikadhalika wataalamu hawa watapatikana  kupitia programu maalumu ya ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni ambayo hutolewa na Bakita ili kutengeneza wajuzi au walimu wabobevu ambao watajikita katika kutoa mafunzo ya Kiswahili kwa wageni kwa kutumia mkabala wa kimawasiliano.

Hivyo, hii ni fursa kubwa kwa wamilisi na wataalamu wa Kiswahili ambayo inazalishwa kupitia mpango mkakati wa kubidhainisha Kiswahili. Wataalamu wa Kiswahili wanapaswa kujisajili katika kanzidata ya Bakita na Bakiza. Pia, kuhakikisha kuwa wanaujuzi wa kutosha katika ufundishaji Kiswahili kwa wageni ambao unaukiliwa na kupata mafunzo maalumu ya ufundishaji Kiswahili kwa wageni yanayotolewa na Bakita na Bakiza: kwa kufanya hivyo, wataweza kunufaika fursa hii ‘adhimu’ inayozalishwa kupitia mpango mkakati wa kitaifa wa kubidhainisha Kiswahili.

Taaluma za Tafsiri na Ukalimani

Hizi ni taaluma mbili tofauti , ingawa zina uhusiano mkubwa sana na inaashauriwa unapopata ujuzi taaluma mojawapo kati ya hizi ni vyema ukajifunza nyingine ili kujenga ujuzi na kuweza kutofautisha upekee na utofauti wa taaluma hizi: Tafsiri imejiegemeza katika uhawilishaji wa maana, ujumbe uliopo kwenye maandishi kutoka lugha moja (chanzi) kwenda lugha nyingine (lengwa) kwa kuzingatia muundo husika, ilihali ukalimani ni taaluma iliyojiegemeza katika uhawilishaji wa maana au ujumbe kwa mfumo wa sauti- papo kwa papo ( immediacy) kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.

Kupitia mpango mkakati wa kubidhaisha Kiswahili taaluma hizi ni mojawapo ya fursa zinazojiibua kutokana na programu maalumu zinazoendeshwa na Bakita na Bakiza ambazo huwapiga msasa kwa kuendesha kozi maalumu za kivitendo kwa kutumia vifaa vya kieletroniki ili kuongeza tajiriba na ujuzi kwa wataalamu wa Kiswahili katika tafsiri na ukalimani  ambao watatumika katika mahitaji ya sekta mbalimbali ambazo zinahitaji uwepo hivyo kujitengezea soko la ajira.

Vyombo vya habari

Ukuaji na ueneaji wa Kiswahili umechagngiwa sana na vyombo vya habari hii ni kutokana na maudhui ambayo yanayowasilishwa na vyombo hivi hutumia lugha ya Kiswahili.

Pia huibua maneno mapya ambayo huongeza msamiati wa lugha hivyo kukuza lugha ya Kiswahili mikakati iliyowekwa na mabaraza ya Kiswahili ni kunoa wanafunzi wa Kiswahili ili kuzalisha wajuzi katika taaluma ya uandishi na uhariri ambao watahusika katika kuzalisha maudhui na kuweza kuyahakiki maudhi hayo kwa Kiswahili hivyo kupanua wigo mpana katika vyombo vya habari.

Kwa ujumla, wataalamu watakaozalishwa watapata nafasi katika vyombo vya habari ili kuweza kuzalisha maudhui na kuweza kuyahakiki kwa Kiswahili kwa kuzingatia usanifu wa lugha ya Kiswahili yaani kutumia Kiswahili fasaha kwa mujibu wa kanuni na sheria zinazotawala matumizi ya Kiswahili.

Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA)

Mpango mkakati wa kubidhaisha Kiswahili umedhamiria kutoa programu zinazohusu Tehama kupitia mabaraza, asasi, na vyama vinavyozijishugjulisha na Kiswahili ili kukidhi na kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa muktadha wa sasa na tunakokwenda.

Hivyo mpango huu utazalisha wataalamu wenye ujuzi na masuala ya Tehama ambao watatumika katika majukumu mbalimbali ya Mabaraza na asasi anuwai za Kiswahili ikiwemo kufanya katika kazi tovuti na mitandao ya kijamiii mathalani ‘Facebook, Twitter, na Instagram’.

Wataalamu hao watahusika kutoa maudhui mbalimbali yanayohusu kiswahili ambayo yameandaliwa na mabaraza au asasi za Kiswahili kwaajili ya kuuhabarisha umma.

 Wamilisi wa Kiswahili wanatakiwa kusoma programu za Tehama zinazotolewa za mabaraza na Asasi za Kiswahili ili kujijengea ujuzi ili kunufaika na fursa za Kiswahili zinazojiegemeza katika Teknolojia ya habari na mawasiliano kupitia mpango mkakati wa kubidhainisha Kiswahili.

Uuzaji wa machapisho

Mabaraza ya Kiswahili kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mpango mkakati wa kuibidhaisha Kiswahili umedhamiria kutengeneza fursa za ajira kwa wajuzi wa taaluma za Kiswahili.

 Mpango mkakati wa kuibidhaisha Kiswahili umepanga kuanzisha vituo vya kuuzia machapisho mbalimbali yanayohusu utamaduni  wa Kiswahili kwa wazawa na wageni kutoka nje ya nchi katika viwanja vya ndege:Dar es Salaam, Kilimanjaro, na Zanzibar.

Vituo hivi vitakuwa na wafanyakazi ambao wataajiriwa na mabaraza kwa kushirikiana na Serikali zote mbili hivyo, itafungua milango ya ajira kwa wataalamu wa Kiswahili kunufaika na fursa hii, kadhalika itaongeza mapato kwa mabaraza ya Kiswahili na kwa Serikali kupitia manunuzi ya machapisho hayo.

Mbali na hayo, Bakita na Bakiza wamedhamiria kuanzisha maktaba ya mabaraza hayo ili kutoa fursa kwa wazawa na wageni kupata maeneo maalumu ya kujifunza maarifa mbalimbali ya Kiswahili kupitia machapisho ya Kiswahili katika nyanja zote: Kiuchumi, kisiasa, kijamii, na kitamaduni.

 Mpango huu utahitaji wafanyakazi watakaohudumu katika maktaba hizo yaani “wakutubi’, kadhalika maktaba hizo zitakuwa na maeneo maalumu ya kuuza machapisho mbalimbali ya Kiswahili hivyo, itatengeza faida kwa mabaraza ya Kiswahili kupata mapato na kufungua milango ya ajira kwa wataalamu wa Kiswahili.

Author: Gadi Solomon